28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

JANGA LA CORONA: Viongozi wazuia mikusanyiko, wanasayansi watafuta suluhu huku wahalifu wanatapeli

Na MWANDISHI WETU

HALI ilivyo sasa ni kwamba kila nchi inapambana kadri iwezavyo kuhakikisha kuwa inadhibiti kusambaa kwa virusi vya corona- covid 19 vinavyosababisha maradhi ya kukohoa, mafua makali, mafindofindo na kushindwa kupumua.

Hali hii imeifanya Tanzania kuzuia baadhi ya shughuli kama michezo, harusi, kufunga shule, kusitisha mbio za mwenge na mikusanyiko mingine inayoweza kuchangia kusambaa kwa maambukizi.

Sio Tanzania tu, nchi nyingi duniani zimelazimika kuweka amri ya kutokuwapo kwa mikusanyiko baina ya watu ‘lockdown’, ili kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona yaliyoathiri watu wengi duniani na hata wengine kupoteza maisha.

Amri ya kukaa nyumbani ‘lockdown’ imekuwa ikiwekwa na nchi mbalimbali zilizokumbwa na mlipuko wa coronavirus kwa kiwango tofauti kulingana na na mlipuko na kasi ya kusambaa kwake katika nchi husika.

‘Lockdown’ imewafanya watu kubadili mtindo wao mzima wa maisha ili kuzingatia sheria.

Swali ni je, Watanzania wanaweza kuzingatia agizo la aina hii iwapo serikali itatangaza ‘lockdown?

Kukaa nyumbani kunamaanisha kwamba watu hawaruhusiwi kabisa kutoka majumbani mwao au inaweza kuwa ni kusitisha baadhi ya shughuli za umma na matembezi ya watu kudhibitiwa kwa kiwango fulani.

Kwa mfano, Januari 23, China iliweka amri kamili ya kukaa nyumbani dhidi ya wakazi wa Jiji la Wuhan, lenye watu milioni 11, ambako virusi hivyo inadhaniwa kuanzia, ilikuwa ni amri kamili ya kukaa nyumbani.

Ndani ya jiji, usafiri wa umma ulizuiwa, magari binafsi yalizuiwa kuendeshwa barabarani mara nyingi, isipokuwa pale yanapokuwa sehemu ya kampeni ya vita dhidi ya virusi vya corona.

Italia pia ilitangaza amri kamili ya watu kukaa nyumbani baada ya kuwa na kasi ya maambukizi ya coronavoirus.

Amri hiyo iliwataka wakazi wa jiji hilo kutosafiri kuingia ama kutoka nje ya jiji hilo, hata wale waliokuwa na sababu za kimatibabu au kwa sababu za kibinadamu hawakuruhusiwa kutoka.

‘Lockdown’ ilianza kutekelezwa kwa mara ya kwanza kaskazini mwa nchi, kabla ya kutekelezwa kitaifa na serikali imewataka watu milioni 60 wa Italia kubakia majumbani mwao pale inapowezekana.

Ufaransa pia ilitoa amri kamili ya kukaa nyumbani. Kulingana na amri hiyo, raia wanaotoka majumbani mwao lazima wabebe waraka unaoelezea ni kwanini wametoka, huku nchi hiyo ikiwa imeweka faini ya €135 ($150; £123) kwa yeyote atakayekiuka amri ya kutoka bila sababu.

Rais Emmanuel Macron, awali aliwaamuru watu kubaki majumbani mwao na waende nje tu pale wanapoenda kufanya majukumu muhimu. 

Anasema: “Tuko vitani… hatupambani na jingine lolote lile wala nchi yetu wenyewe. Lakini adui yuko hapa, haonekani, hawezi kuguswa na anasonga mbele.”

Amri hii inaweza kuwalazimu watu kufunga biashara zisizokuwa za lazima, huku ikiwaruhusu wengine wanaofanya biashara za vyakula na mahitaji na bidhaa nyingine muhimu za nyumbani, maduka ya dawa, benki na vituo vya mafuta ya petroli kuendelea kufunguliwa.

Tunaona hali ambavyo inaweza kuwa mbaya iwapo Tanzania itafikia hatua hiyo, swali la kujiuliza ni je, kwa maisha ya kawaida ya wananchi wengi, watamudu kujaza vyakula ndani ili wasiweze kutoja nje? Hii ni kazi ngumu, jambo la kufanya ni kuzingatia masharti tunayopewa na wataalamu ili nchi yetu isiweze kufikia hatua hiyo.

Idadi ya maambukizi kwa hapa kwetu na hata nchi jirani ya Kenya bado ni ya kiwango cha chini, ndio maana hadi sasa viongozi hawajachukua hatua ya kutoa amri ya kukaa nyumbani – lockdown.

Hata hivyo, kasi ya kuenea kwa maambukizi ya coronavirus inawatia hofu baadhi ya raia wa Tanzania ambapo kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakiitaka serikali kuchukua hatua kubwa zaidi ikiwamo kufunga mipaka na hata watu kuzuiliwa kutoka ndani.

Kilichofanyika kwa Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda katika kukabiliana na janga hili ni kutolewa kwa maagizo au melekezo kwa raia.

Ilichofanya Tanzania kwa sasa ni kuwashauri watu wasiokuwa na safari za lazima kusitisha safari zao kwenye nchi zenye maambukizi.

Taasisi zote zikiwemo shule, hoteli, maduka ya biashara, nyumba za kulala wageni, makanisa, misikiti, ofisi za umma na binafsi, vituo vya kutolea huduma za afya, taasisi za fedha, vyombo vya usafiri pamoja na maeneo ya mikusanyiko ya watu kama vile masoko, viwanja vya michezo na vituo vya abiria kuweka vifaa vya kunawia mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni au maji yenye dawa kwa ajili ya kuhakikisha usafi wa mikono.

Sharti jingine ni kuweka maji yenye dawa ya chroline katika mageti ya kuingia katika hifadhi zote kwa ajili ya kusafisha mikono ya watalii na waongoza wageni.

Kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono, kukumbatiana, kubusu, kuepuka kushika pua, mdomo na macho.

Hospitali zote nchini za serikali na zisizo za serikali zimetakiwa kuweka zuio la idadi ya watu wanaokwenda kuwaona ndugu zao. Kwa maelekezo ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,  ni kwamba wageni wa kumuona mgonjwa wasizidi wawili kwa siku kwa kila mgonjwa mmoja.

Wananchi pia wametakiwa kutoa taarifa kwa vituo vya afya iwapo watamuona mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Covid- 19.

Hivi juzi, imetangaza kupiga marufuku kuwatembelea wafungwa. 

Hatua zilizochukuliwa Kenya

Kwa upande wa Kenya, ambayo sasa ina visa saba vya coronavirus hali si tofauti na Tanzania, kwani baada ya ilipopata kisa coronavirus Wakenya walipewa maagizo na katika jitihada za kuudhibiti Rais Uhuru Kenyatta, alitoa maagizo ya kuepuka mikusanyiko ikiwamo maeneo ya kuabudu.

Kupunguza mikusanyiko ya kijamii kama harusi na mazishi, masharti ambayo yanapaswa kuzingatiwa na wanafamilia.

Kuepuka maeneo yenye msongamano wa watu ikiwamo maduka ya jumla na maeneo ya burudani. Kupunguza mikusanyiko katika maeneo ya usafiri wa umma na kwingineko.

Kuwapo ukomo wa wageni wanaotembelea wagonjwa waliolazwa katika hospitali za umma na binafsi. 

Rwanda

Hatua zilizochukuliwa na Rwanda ni pamoja na kuzuia mikusanyiko ya watu na kuhimiza usafi.

Waziri wa Afya Rikali ya Rwanda, imetangaza kuchukua hatua kadhaa za dharura kukabiliana na janga hilo, saa kadhaa baada ya kutangaza kwamba raia mmoja wa India aliyewasili nchini humo Machi 8, kuwa na virusi vya corona.

Nchi hiyo ambayo imekuwa na idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya coronavirus kwa upande wa Afrika Mashariki ambapo wagonjwa wamefikia 11 imetoa maagizo kwa umma kufungwa kwa maeneo ya kuabudu na sehemu zote za umma.

Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA), pia limetangaza kwamba michuano yote kwa sasa itafanyika bila kuhudhuriwa na mashabiki katika viwanja vya michezo, huku shirikisho la mpira wa mkono nchini humo likiahirisha michezo yake yote.

Raia wametakiwa kunawa mikono yao mara kwa mara na safari za kuingia na kutoka nchini humo zimezuiwa kwa muda.

Uganda

Licha ya kwamba nchi hii bado haijaripoti kisa chochote cha maambukizi ya coronavirus, imechukua hatua za kudhibiti maambukizi huku serikali ikitoa maagizo kwa raia ikiamini yatasaidia kudhibiti maambukizi.

Serikali ya Uganda iliweka sera ya karantini ya lazima kwa wasafiri wanaowasili nchini humo kutoka mataifa 16 yaliyo katika ‘hatari zaidi’ ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Uingereza, Marekani na nchi kadhaa za Ulaya zinatajwa kuwa miongoni mwa mataifa yatakayoathiriwa na sera hiyo mpya ya usafiri nchini Uganda.

Awali serikali pia ilisema wasafiri wanaowasili katika uwanja wa kimataifa wa Entebbe watakuwa wakipuliziwa dawa.

Ni dhahiri kwamba visa vya coronavirus katika mataifa ya Afrika Mashariki ni ndogo, ikilinganishwa na maeneo mengine duniani. 

Janga hili litakwisha?

Swali la kujiuliza ni iwapo ugonjwa huu wa corona unaweza kuisha. Mataifa tajiri ikiwamo Marekani imekuwa ikipambana kuhakikisha dawa ya corona inapatikana, lakini hadi sasa hali bado ni mbaya licha ya kwamba kuna matumaini.

Bado watu hawajafahamu kwa kina ni lini hasa hali hii ya hofu dhidi ya corona itaondoka.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson anaamini kuwa mlipuko huu unaweza kupata chanjo ndani ya wiki 12 zijazo. Idadi ya kesi za corona nayo zitaanza kupungua katika miezi mitatu ijayo, hivyo bado ni mbali kufikia hatima ya janga hili.

Mlipuko wa ugonjwa huu unaweza kuchukua muda mrefu kuondoka, inawezekana kuchukua hata mwaka mzima kwa sababu bado watu watalazimika kusafiri kutoka taifa moja kwenda jingine.

Sasa hivi shughuli za kijamii na kiuchumi zimedorora na zinatarajia kuathiri dunia kwa kiwango kikubwa.

“Tuna tatizo kubwa na kuondoka katika tatizo hili pia ni changamoto kubwa,” anasema bwana Mark Woolhouse, Profesa wa magonjwa ya maambukizi katika Chuo Kikuu cha Edinburgh.

“Tatizo halipo Uingereza peke yake, hakuna taifa ambalo lina mikakati ya kujinasua kutoka katika janga hili.”

Ni changamoto kubwa kwa wanasayansi na janga kubwa kwa jamii kwa ujumla, lakini njia tatu pekee zinatajwa kuweza kukabiliana na tatizo hili.

Njia hizo ni pamoja na chanjo, watu wengi kuwa na kinga ya kuepuka maambukizi au kubadili mifumo ya maisha.

Njia hizo zinaweza kuzuia maambukizi kusambaa kwa wingi, ambapo chanjo inatarajiwa kupatikana ndani ya miezi 12 hadi 18.

Chanjo hii inaweza kumpa mtu kinga kutokuwa ugonjwa endapo akikumbana na maambukizi ya virusi.

Watu wengi wakipata chanjo kama kinga, angalau kwa asilimia 60, basi virusi haviwezi kusababisha milipuko kutokea.

Mgonjwa wa kwanza alipewa chanjo kama jaribio nchini Marekani wiki hii baada ya watafiti kusema kuwa waliruhusiwa kuacha kutumia mlolongo ambao huwa wanatumia kila wakati kwa kutumia vipimo vya wanyama.

Utafiti wa chanjo unafanyiwa kwa haraka lakini hakuna uhakika ni lini wataweza kufanikiwa kupata kinga hiyo duniani kwa ujumla.

Kama chanjo itawezekana kupatikana kama ilivyopangwa kwa miezi 12 hadi 18, basi kila kitu kitaenda sawa.

Wahalifu mtandaoni waongeza hofu

Wataalamu wa masuala ya usalama wanasema corona imefanya wahalifu wa mtandaoni kutumia mwanya huu kutapeli watu.

Wahalifu hao wanawalenga watu binafsi pamoja na sekta mbalimbali kama usafiri, utalii, afya, elimu, bima na shughuli nyingine.

Barua pepe za ulaghai ambazo zinaandikwa kwa lugha ya Kiingereza, Kifaransa, Kiitaliano, Kijapani na Kituruki zimebanika.

Kuna barua ambazo zinaelekeza wapi watu wanaweza kupata tiba ya corona. Watafiti katika makosa ya kihalifu waligundua barua pepe ambayo hawakuielewa kutoka kwa wateja Februari, mwaka huu.

Ujumbe ukiwa ulitoka kwa daktari aliyedai kuwa kuna chanjo iliyobainika kutengenezwa na serikali ya China na Uingereza, ikiwataka watu kufungua nyaraka hiyo yenye maelezo kuhusu chanjo.

Barua pepe zipatazo 200,000 zimetumwa kwa wakati mmoja kwa watu tofauti. 

“Tumeona mawasiliano mengi kwa siku kadhaa ambazo zinafanya kampeni kuhusu corona ambayo haieleweki, wengi wakiwa wanawaogopesha watu ili kuwashawishi wafungue nyaraka hiyo,” anasema Sherrod DeGrippo kutoka kampuni inayofanya utafiti wa vitisho hivyo vya mtandao.

Utafiti unasema kuwa utapeli huo unafanyika kila siku. Ukweli ni kwamba, kampeni hizi za uhalifu mtandaoni zinapata mapokeo yaliyogawanyika.

Muhimu ni kwamba watu wasifungue nyaraka hizo ambazo zinazunguka mitandaoni kwa lengo la kutapeli.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles