32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JANGA JIPYA LA ELIMU LAIBUKA NCHINI

*Maelfu wafeli kidato cha pili, darasa la nne ‘vibomu’ vyatawala

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


 

kufeli kidato cha piliKATIKA kile kinachoonyesha kuwa ni janga jipya kwenye  sekta ya elimu, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde, amesema wamebaini udanganyifu kwenye Mtihani wa Upimaji Kitaifa  wa Kidato cha pili na darasa la nne.

Amesema katika mtihani wa kidato cha pili imebainika kulikuwa na mamluki waliojifanya watahiniwa na kuingia darasani kufanyia wanafunzi mitihani hiyo ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Dk. Msonde, alisema watahiniwa 31 wamefutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha pili uliofanyika Novemba mwaka jana kutokana na udanganyifu huo pamoja na   kuingia na karatasi za majibu kwenye vyumba vya mtihani.

Alisema kwenye mtihani kama huo uliofanywa na wanafunzi wa darasa la nne, yamefutwa matokeo kwa watahiniwa 58 waliofanya udanganyifu wa aina mbalimbali.

“Wasimamizi walibaini pia mamluki waliingizwa ndani na kufanya mitihani katika baadhi ya shule,” alisema Dk. Msonde.

Alisema watahiniwa wa kidato cha pili waliofutiwa matokeo yao  watarudia mtihani huo mwaka huu.

Alisema NECTA imezishauri mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua  wote waliohusika kusababisha udanganyifu huo.

Kuhusu darasa la nne, alisema Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 58 waliobainika kufanya udanganyifu hivyo wataruhusiwa kurudia mwaka huu.

Alisema ilizoeleka kuona udanganyifu wa aina hiyo ukifanywa katika mtihani wa kidato cha nne na kwa kiasi kidogo darasa la saba.

Maelfu wafeli

Dk, Msonde alisema  wanafunzi  36,737 (asilimi 8.98) watakariri kidato cha pili mwaka huu kutokana na kushindwa mtihani huo.

Alisema  shule za serikali zimefanya vibaya zaidi ambako tisa kati ya 10 za mwisho zimetokea mkoani Mtwara.

Wanafunzi waliofanya mtihani huo ni 410,519, kati yao waliopata wastani wa kuanzia alama 30 na kuendelea ni 372,228  (asilimia 91.02) ambao wataendelea na kidato cha tatu.

Kwa   darasa la nne, wanafunzi 67,547  (asilimia 6.64) waliopata alama E kwenye Mtihani wa Upimaji wa Taifa wa (SFNA) nao watakariri darasa hilo.

Dk. Msonde akitangaza matokeo hayo jana, alisema kwa   kidato cha pili, kati ya hao waliofaulu, wasichana ni 189,161 (asilimia 90.27) na wavulana 183,067 (asilimia 91.80).

Alisema matokeo hayo yanaonyesha ufaulu wa wanafunzi katika masomo ya msingi ya Uraia, Historia, Jiografia, Fizikia, Biolojia, Kiswahili na Hisabati umepanda.

Dk. Msonde alisema ufaulu kwa somo la Kiingereza umeshuka ikilinganishwa na mwaka 2015.

“Somo la Kiswahili limefanya vizuri katika mtihani wa mwaka jana ambako asilimia 90.06 ya wanafunzi wamefaulu, somo lenye ufaulu wa chini zaidi ni Hisabati ambalo lina ufaulu wa asilimia 21.55,” alisema.

Dk. Msonde alisema mwaka 2015 wanafunzi 324,068  (asilimia 89.12) ndiyo ambao walifaulu kwenda kidato cha tatu.

“Katika mtihani wa 2016 waliandikishwa   wanafunzi 435,075 kufanya mtihani huo, wasichana walikuwa 221,086 (asilimia 50.82) na wavulana 213,989 (asilimia 49.18).

“Kati ya wanafunzi hao waliosajiliwa, 410,519 (asilimia 94.36) walifanya mtihani huo, wasichana walikuwa 210,345 (asilimia 95.14)  na wavulana 200,174  (asilimia 93.54),” alisema.

Aliongeza:  “Wanafunzi 24,556  (asilimia 5.64) walishindwa kufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo utoro na ugonjwa.

Dk. Msonde alisema idadi ya watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa madaraja I,II na III ni 178,115  (silimia 43.55) wasichana wakiwa 78,466 (asilimia 37.45) na wavulana 99,649  (asilimia 49.97).

Shule 10 bora

Alisema shule 10 bora zinaongozwa ma Shule ya Wasichana St.Francis (Mbeya), Kilimanjaro Islamic (Kilimanjaro), Kaizirege Junior (Kagera), Canossa, Thomas More Machrina na Shamsiye (Dar es Salaam), Twibhoka Boys (Mara), Marian Boys (Pwani), Tengeru Boys na Precious Blood (Arusha).

Shule zilizofanya vibaya

Alizitaja shule 10 kutoka mwisho kuwa ni  Chingungwe, Malocho za Mtwara, Nywelo ya Tanga, nyingine ni Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukokoda, zote za Mtwara.

Watahiniwa 10 bora kitaifa

Wanafunzi waliofanya vizuri, majina ya shule na mikoa zilizopo kwenye mabano kwa kuanza na nafasi ya kwanza ni  Teckla Haule (Canossa, Dar es Salaam), Joseph Kalabwe (Kwema Modern, Shinyanga), Mirabel Matowo (Canossa, Dar es Salaam).

Wengine ni Hamida Kihiyo (St. Aloysius, Pwani), Rachel Sogoja (Heritage, Pwani), Clare Hamissi, Roselyn Kissaka, Joy Kimambo, Venastra Mringo na Babymaisara Kimazi (wote wa Feza Girls, Dar es Salaam).

Wasichana 10 bora

Dk. Msonde aliwataja wasichana 10 bora kuwa ni Teckla Haule, Mirabel Matowo (Canossa), Hamida Kihiyo (St. Aloysius), Rachel Sogoja (Heritage), Clare Hamissi, Roselyn Kissaka, Joy Kimambo, Venastra Mringo, Babymaisara Kimazi (wote wa Feza Girls) na Janeth Nandi (Marian Pwani).

Wavulana 10 bora kitaifa

Aliwataja walioshika nafasi 10 bora kitaifa kuwa ni Joseph Kalabwe (Kwema modern), John Bugeraha, Evance Munishi, Isack Julius, Avith Kibani, Emmanuel Dismas, Harry Mshana na Salim Mchomvu (wote wa Marian Boys), Lorian Njian (Kaizirege Junior) na Omega Lugata (Marian Boys).

Darasa la nne

Kwa   mtihani wa darasa la nne, Dk. Msonde alisema matokeo yanaonyesha somo lililofanya vizuri zaidi ni stadi za kazi, Haiba na Michezo ambako ufaulu wake ni asilimia 94.67.

Alisema somo walilofaulu kwa kiwango cha chini kulinganisha na masomo yote ni Kiingereza lenye ufaulu wa wastani wa asilimia 72.51.

“Wanafunzi 1,054,191 walisajiliwa kufanya upimaji huo wasichana wakiwa ni 542,071 (asilimia 51.42) na wavulana 512,120  (asilimia 48.58).

“Kati ya hao waliosajiliwa, wanafunzi 1,017,776  (asilimia 96.55) ndiyo ambao walifanya upimaji. Kati yao wasichana ni 526,612  (asilimia 97.15) na wavulana 491,164  (asilimia 95.91),” alisema.

Aliongeza:  “Wanafunzi 36,415 (asilimia 3.45) hawakufanya upimaji kati yao wasichana ni 15,459  (asilimia 2.85) na wavulana 20,956  (asilimia 4.09)”.

Alisema   wanafunzi 950,167 (asilimia 93.36) ya waliofanya upimaji huo wamepata alama A,B,C na D na  wanafunzi 67,547 ( asilimia 6.64) wamepata alama E ambayo ni ufaulu usioridhisha.

Alitaja mikoa 10 iliyofanya vizuri katika upimaji huo ni Kagera, Kilimanjaro, Geita, Njombe, Iringa, Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Mwanza na Katavi.

Halmashauri zilizofanya vizuri ni Bukoba, Mji Makambako, Tanga mjini, Chato, Mafinga mji, Mufindi, Ilala, Biharamulo, Hai na Muleba.

“Shule 10 bora ni St Leo The Great na Acacia Land ( za Tabora), Kadama, Waja Spring, Msasa (za Geita), Twibhoki (Mara), St. Peter Claver (Kagera), Chalinze Modern Islamic (Pwani), Imani na Mudio Islamic ( Kilimanjaro).

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles