25 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Jamii yaaswa kuhusu unyanyasaji wa kingono wakati huu wa corona

Na Mwandishi Wetu

JAMII imetakiwa kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda wanawake na wasichana wadogo kipindi hiki cha janga la corona.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi imesema kuwa watoto wa kike wapo katika hatari ya kupata mimba za utotoni na aina nyingine za ukatili wa kijinsia wakati huu ambao wapo nyumbani.

“Watoto (wa kike na wakiume)  wanabaki nyumbani, na wazazi wao wanakwenda kazini. Katika hali hii unyanyasaji wa kingono unaweza kujitokeza na kusababisha mimba za utotoni”Dada Lilian amesema.

Ripoti hiyo ya TGNP inaonyesha kuwa takribani asilimia 60 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hutokea majumbani, na wanaofanya vitendo hivyo ni aidha ndugu wa karibu au majirani.

“Kwa ujumla, ukatili wa kijinsia huongezeka sana wakati wa majanga kama haya, si tu kwa watoto bali pia kwa wanawake” Lilian amesema.

Taarifa yake inaonyesha kuwa kuwa wanawake wengi nchini wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi, wakifanya shughuli mbalimbali kama vile mama ntilie, biashara masokoni, viwandani, majumbani, kazi ambazo zinawalazimisha kutoka mazingira ya nyumbani kwao na kukutana na watu, mara nyingi katika mazingira yenye misongamano mikubwa.

Lilian amesema kuwa hali hii inawaweka wanawake katika mazingira hatarishi ya kupata virusi vya Corona -COVID 19, na akaongeza kuwa ni muhimu sana kwa sasa kuweka mikakati madhubuti ya kuwalinda kwa kuwafikia, na kuwapelekea huduma na elimu sahihi huko waliko ili waweze kujikinga.

Janga la  virusi vya corona limeibua changamoto mpya katika familia na jamii kwa ujumla, na hasa kwa watoto wa kike ambao kwa sasa wapo nyumbani baada ya shule kufungwa hivi karibuni.

 “Kwa upande wa Afya ya Uzazi ya mama na mtoto, ukweli wakitabibu kuhusu mwanamke mwenye ujauzito na aliyetoka kujifungua ni kuwa, kinga zake si imara sana hususan kwa kipindi anaponyonyesha. Kwa hospitali zilizo na wauguzi wanawake wazazi wa chini ya mwaka mmoja, tunashauri kuwa wasipangiwe majukumu ya kuhudumia wagonjwa wa Corona” Amesema  Lilian.

Ameongeza kusema kuwa katika huduma za kliniki kwa wajawazito na watoto, ambapo mara nyingi huwa na msongamao wa watu, ni vyema kusisitiza kuhusu taratibu za kujikinga ikiwemo kunawa mikono, kupata huduma kwa kukaa mbali kwa mita moja toka mtu na mtu, huku wakijipanga kwa foleni.

Kwa kujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyu was TGNP, janga la corona limechukua umakini mkubwa sana wa watoa huduma wa afya katika kuhakikisha kuwa ugonjwa unazuilika na kuwatibu wale wanaokutwa na ugonjwa na hata serikali kutenga hospitali maalumu za kuwahudumia.

“Ni muhimu kuhakikisha mizani ya utoaji huduma hospitalini imekaa sawa kwa kuhakikisha pia huduma za kina mama wajawazito na watoto zinaendelea kupewa kipaumbele ili kuendelea kupunguza vifo vya kina mama na watoto vitokanavyo na uzazi” Amesema .

 Amewataka wazazi wote, baba na mama kuhakikisha kuwa wanawajibika kujikinga wanapokuwa katika shughuli zao zinazowalazimu kutokaa nyumbani kwa sababu ikitokea mzazi ameambukizwa akirudi nyumbani ataweza kuwaambukiza watoto, na hivyo juhudi ya sekikali kuwalinda watoto haitokuwa na maana. 

  Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Ajira Duniani (ILO) zilizotolewa mwaka 2006, zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wapo katika ajira zisizo  rasmi kama vile masokoni ambapo kuna mikusanyiko mikubwa sana jambo ambalo linawaweka katika hatari kubwa sana ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu.

 Taarifa ya UNESCO ya 2019, kiwango cha elimu kwa watu wazima ni asilimia 77.82, ambapo wanaume ni asilimia 83.2, na wanaobakia ni wanawake.

Takwimu hizi ni ushahidi wa wazi kuwa wanawake wameachwa nyuma katika masuala mbalimbali.

Tofauti hiyo ya wanawake kuwa nyuma utaiona pia katika nyanja ya ufikiwaji wa taaarifa sahihi kwa wakati mfano magazeti, radio, televisheni na  namitandao ya kijamii.

Hali hii kwa kiasi kikubwa inatokana na mifumo wa jamii zetu ya kutokuwa na mgawanyo sawa wa majukumu.

Wanawake kwa kiasi kikubwa wameelemewa na majukumu ya kulea familia na kazi za kutoa huduma  ambazo zinapelekea kukosa muda kabisa  wa majukumu ya kiuchumi, kisiasa, na hata kupata taarifa sahihi na kwa wakati.

Kwa kipindi hiki cha janga la COVID-19, upatikanaji wa taarifa sahihi ni haki kwa kila mwananchi, hivyo ni muhimu mbinu zinazotumika ziangalie mahitaji ya taarifa kwa makundi mbalimbali ya kijamii pamoja na vyombo na muda sahihi wa kupeleka taarifa kwa makundi hayo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,538FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles