JAMII ISHIRIKISHWE KIKAMILIFU KUSHUGHULIKIA NIDHAMU ZA WANAFUNZI

0
466

Na Christian Bwaya


IMEJENGEKA dhana kwamba adhabu ndiyo namna bora ya kumsaidia mwanafunzi kujirudi. Mwanafunzi anapokosea, walimu pamoja na jamii inayomzunguka wanaona njia sahihi ya kumrekebisha ni kushughulika naye moja kwa moja. Tunamwadhibu mwanafunzi aliyekosea pasipo kufikiri namna ya kubadili mazingira ambayo kimsingi ndiyo yanayochangia kumtengeneza kuwa vile alivyo.

Pamoja na wingi wa adhabu tunazoamini zinawafaa wanafunzi, bado tumeendelea kuwa na orodha ndefu ya matatizo ya kinidhamu yanayotajwa kutamalaki katika shule zetu. Tumeadhibu lakini bado utovu wa nidhamu kwa wanafunzi umeendelea kuwa tatizo. Shule zenye kuweka msisitizo katika adhabu kali na kubwa kwa wanafunzi hazijaonesha tofauti kubwa ya kinidhamu. Katika mazingira kama haya swali linakuwa suluhisho ni lipi? Kuongeza uzito wa adhabu kwa wanafunzi au kubadili mbinu?

Juma lililopita nilizungumza kwa kirefu na mwalimu mmoja msomaji wa gazeti hili. Kwa maoni yake, adhabu zimeshindwa kuleta matokeo yanayotarajiwa. Anasema kadri wanafunzi wanavyochapwa ndivyo wanavyoendelea kuonesha ukosefu mkubwa zaidi wa maadili. Nakubaliana naye kwa sababu moja kubwa.

Pamoja na umuhimu wa adhabu kwa mwanafunzi, wakati mwingine adhabu hizi hutolewa katika mazingira yanayojenga hisia za kisasi na chuki kwa wanafunzi. Hisia hizi zinaweza kutokana na ukweli kwamba walimu na wazazi wamewekeza nguvu zao katika kuadhibu kuliko kumsaidia mwanafunzi kujenga tabia mbadala. Mwanafunzi aliyekosea, anaadhibiwa pasipo kuonyeshwa namna nyingine ya kutenda. Hata pale anapoonekana kubadilika, haichukui muda mrefu kurejea tabia yake ya awali.

Tunahitaji suluhisho la muda mrefu. Pengine kubadili mbinu zinazotumika kuwasaidia wanafunzi inaweza kuwa sehemu ya suluhisho la muda mrefu. Katika makala haya, ninapendekeza ushirikishwaji mpana wa jamii kama namna bora zaidi ya kuwasaidia wanafunzi kubadilika.

Nianze kwa kukumbusha kwamba mwanafunzi ni sehemu ya jamii anamoishi. Karibu kila anachojifunza – kiwe chema au kiovu –kimetokana na jamii yake. Jamii ni pamoja na mtandao wa marafiki alionao mwanafunzi; watu maarufu anaojipambanua nao mwanafunzi; majirani na watu mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wanaathiri maisha yake. Hawa wote kwa pamoja ndio wanaowajibika kutengeneza tabia tunazoweza kuziona kwa wanafunzi.

Aidha, upo ukweli kwamba utovu wa nidhamu wanaouonesha wanafunzi ni ujumbe wa hali ya mambo katika familia yake. Wanachokifanya watoto shuleni ni kama kupaza sauti –bila wao kujua – kwamba kuna matatizo nyumbani yanahitaji ufumbuzi. Kwa mfano, wapo wanafunzi wanaokosa ukaribu na wazazi wao. Wanafunzi hawa hawajapata fursa ya kusikilizwa na wazazi wao kujua yale yanayowasibu. Ndani yao kumejaa msongamano wa matamanio yasiyofikiwa sambamba na hofu zisizotatuliwa.

Pia wapo wanaohitaji kusikika. Nafsi zao hajisikii kusikika vya kutosha. Utovu wa nidhamu wanaouonesha ni namna ya kupata usikivu wasioupata nyumbani. Wapo wanaojisikia uduni ndani yao. Wameishi  kwenye mazingira yaliyodhalilisha utu wao. Wametukanwa, wameonewa, wamepuuzwa, wameumizwa. Mioyo yao imejaa hisia za uduni. Wanafunzi hawa wanapokosa nidhamu shuleni, wakati mwingine, ni jitihada za kujaribu kurudisha hisia za mamlaka wasiyokuwanayo.

Wanafunzi wa jinsi wanapokuja shuleni, wanahitaji kukutana na mazingira ya watu wanaoweza kuwasaidia kujisikia tofauti. Wanahitaji mazingira yanayowaonesha mbadala kuliko kushutumu kisichokubalika. Bahati mbaya ni kwamba shuleni nako, wanakutana na walimu wenye mtazamo wa kuadhibu zaidi kuliko kuwaonesha tabia mbadala. Adhabu, katika mazingira kama haya, zinaendelea kukuza kile kinachojaribu kukomeshwa.

Namna bora ya kuwasaidia wanafunzi hawa ni kuwatazama kama watu walioathirika na mazingira yao badala ya kuwashutumu. Kuwaona kama dalili za udhaifu unaoendelea katika jamii wanamoishi ambao bila kushughulikiwa, jitihada zozote za kumrekebisha mwanafunzi mmoja moja haziwezi kuzaa matunda. Kwa maneno mengine, pamoja na umuhimu wa jitihada zinazomlenga mwanafunzi mmoja moja mwenye matatizo ya kinidhamu, shule zetu zinahitaji kuelekeza nguvu katika kubadili mazingira anayoishi mwanafunzi.

Wazazi wasiachwe nyuma. Hawa ndio wanaoweza kusaidia kuelewa namna gani mazingira ya nyumbani yanachangia matatizo tunayoyaona kwa wanafunzi. Kadhalika, watu wanaogusa maisha ya mwanafunzi kwa namna moja au nyingine, nao wasisahaulike. Ushiriki wa watu hawa, kwa hakika, utafanya kazi ya kumsaidia mwanafunzi iwe rahisi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here