Na Christian Bwaya,
MATUKIO ya watoto wa kike kupata ujauzito yanaongezeka. Kwa mujibu wa Takwimu za Elimu (BEST) wanafunzi 4,718 wa sekondari kwa mwaka 2012 na 3,439 mwaka 2015 walikatishwa masomo yao kwa sababu ya ujauzito. Takwimu kamili hazipatikani lakini kwa elimu ya msingi hali haina tofauti kubwa. Hata hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) linadai kwamba msichana mmoja kati ya sita wenye umri wa miaka 15 hadi 19 wakiwamo wasiokuwapo shuleni hupata ujauzito kila mwaka hapa nchini. Ni wazi kuwa mimba za utotoni ni tatizo kubwa katika jamii yetu.
Aidha, matukio ya mimba yanakwenda sambamba na ongezeko la ngono holela miongoni mwa wanafunzi. Utafiti uliofanywa na Method Kazaura na Melkiory Masatu mwaka 2009, ulibaini kwamba asilimia 32 ya watoto na vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 19 walikuwa wanashiriki vitendo vya ngono. Wengi wao hawana elimu ya afya ya uzazi. Jarida la African Population Studies toleo Na.29 la 2015 linathibitisha matokeo hayo.
Kwa mujibu wa Eunice Muthengi na Abebaw Ferede waliofanya utafiti uliochapishwa na Jarida hilo, idadi kubwa ya vijana hapa nchini wanakosa taarifa za msingi ambazo zingeweza kuwasaidia kufanya uamuzi unaoongozwa na uelewa. Hata hivyo, vijana hawa wanapopatiwa elimu ya afya ya uzazi mapema, asilimia 52 wanaonekana kuweza kuchelewesha uamuzi wa kuanza ngono.
Tunaishi kwenye nyakati zenye uholela mkubwa wa taarifa. Changamoto, hata hivyo, ni kukosekana kwa elimu na huduma za afya ya uzazi kwa vijana. Wazazi, kwa mfano, wameendelea kuogopa kuzungumza kwa uwazi masuala yanayohusiana na ngono kwa imani kwamba ni kinyume na utamaduni wetu. Mtoto huyu anapokwenda shuleni anakutana na walimu wasio na ujasiri wa kuyashughulikia mambo haya kwa uwazi. Katika mazingira haya ya uhaba wa taarifa sahihi katikati ya uholela wa taarifa zinazohimiza ngono, ni wazi uamuzi unaofanywa na wanafunzi utakuwa batili.
Pia, tunafahamu watu wazima wakiwamo wazazi na walimu wameshindwa kuonesha mfano mwema wa kimaadili. Maadili yamebaki kuwa hotuba za majukwaani wakati maisha ya watu faraghani ni jambo jingine kabisa. Wazazi wanaohubiri maadili hadharani, ndio hao hao wanaofuga ‘nyumba ndogo.’ Walimu waliopaswa kuwaelekeza watoto njia sahihi ya kufuata ndio wanaowashawishi wanafunzi wao kushiriki nao vitendo vya ngono. Kwa ujumla, jamii inayomzunguka mtoto inamwaminisha kuwa ngono holela ni sehemu ya maisha.
Jambo la kushangaza ni kwamba mtoto anapoiga yale anayoyaona na kujiingiza kwenye vitendo vya ngono jamii hiyo hiyo inamshangaa. Hukumu inakuwa kubwa zaidi inapotokea binti amepata mimba. Huu ndio unakuwa wakati wa kumkemea mtoto kwamba alichokifanya ni kinyume na maadili. Msichana mwenyewe wakati huo anashangaa imekuwaje kosa lake liwe kubwa kuliko yale anayoyaona yakifanywa na watu wazima wanaomzunguka.
Aliyempa mimba anaamini tatizo ni la binti mwenyewe. Kwa hiyo anamkana. Wazazi, kwa upande wao, wanachukulia mimba kama aibu mbele ya macho ya jamii. Ili kuonekana hawakuzembea, wengi wao nao humshutumu na wakati mwingine kumtenga kuonesha kwamba hawakubaliani na uvunjifu wa maadili uliofanyika.
Msichana huyu akiwa bado katika hali ya kushangaa inakuwaje tumbo linaendelea kuwa kubwa, anajikuta akikabiliana na mkono wa serikali isiyotaka kuona wajawazito wanaendelea na masomo. Watu ambao awali hawakuwa na utaratibu wowote wa kumsaidia kuufahamu mwili wake, wanakuwa wa kwanza kumfukuza ili iwe fundisho wa wanafunzi wengine wasioheshimu maadili.
Mtoto huyu anarudi mtaani akiwa hana mtu anayeweza kuvaa viatu vyake na kujaribu kumsaidia. Kila anayezungumzia tatizo lake anamlaumu yeye. Wengine watasema alijipeleka mwenyewe kwa wanaume. Wengine watasema, ni kiherehere chake kimemponza. Hatua zozote za kumsaidia binti huyu zinatafsiriwa kama kuunga mkono tabia yake mbovu. Kwa kuwa hakuna anayethubutu kuonekana hana maadili, basi kila mtu anashindana kumshambulia ili nay eye aonekane ni mlinzi wa maadili ya jamii.
Ikiwa binti huyu masikini atajifungua salama, atakabiliana na changamoto nyingine ya ndoa. Si wanaume wengi wanaweza kuwa tayari kuanza maisha na mwanamke mwenye mtoto tayari. Katika mazingira kama haya, ni wazi mzazi huyu ataishia kuwa maskini wa kweli kweli atakayelea mtoto fukara kuliko yeye. Kosa kubwa la binti huyu ni kukosa elimu ya afya ya uzazi ambayo ingemwezesha kukabiliana na shinikizo la kushiriki mapenzi kabla ya wakati wake.
Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.