Mwandishi Wetu
WATANZANIA wameanza maadhimisho ya siku 16 za ukatili wa kijinsia jana kwa viongozi na wadau wengine kutoa maelekezo mbalimbali.
Wiki hii ambayo kimsingi ni ya kutafakari na kupinga vitendo vya unyanyasaji ambao kwa kiasi kikubwa wanafanyiwa wanawake na watoto, inapaswa kuwa ya kutafakari zaidi kuhakikisha matukio haya yanapungua au kumalizika kabisa.
Kutokana na hali hiyo, viongozi mbalimbali wa Serikali jana walitoa maelekezo na kukemea vikali tabia hii ambayo huacha maumivu makubwa kwa watu wanaotendewa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akionekana kuguswa na matukio haya, aliagiza maofisa maendeleo ya jamii kusimamia uanzishwaji na uendeshwaji wa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika mikoa na halmashauri ambazo hazijaanzishwa ili kuzuia vitendo hivi hadi ngazi za kata na vijiji.
Anasema dhamira ya Serikali ni kutekeleza kwa vitendo azma ya kukomesha vitendo hivyo ambavyo katika baadhi ya mikoa imekuwa tishio.
Ummy anasema Serikali itaendelea kushirikiana na asasi za kiraia katika mapambano dhidi ya vitendo hivi maeneo mbalimbali ambayo yamekuwa sugu licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa kukemea unyama huu.
Tunaamini agizo la Waziri Ummy linaweza kusaidia kwa sababu linashuka hadi ngazi ya vijiji.
Tunasema hivyo kwa sababu huko ndiko wananchi wengi au kina mama wanapatwa na mateso kutoka kwa waume zao na wanajamii wengine.
Tunapenda madawati haya yawe na watu ambao ni werevu na wenye uwezo mkubwa wa kutoa elimu kwa wananchi kila wakati na si kusubiri hadi mtu akatwe sikio au kuvunjwa mkono.
Tunasisitiza hili kwa sababu kuna mikoa kama Mara, imeota mizizi kila mwaka inakemewa, lakini mabadiliko yamekuwa kidogo. Tunasema hali lazima ikomeshwe.
Pamoja na mambo haya kutokea kwenye familia, lakini kwenye vyuo vya elimu ya juu hali ya rushwa ya ngono katika siku za karibuni imekuwa tishio.
Kama ambavyo tumekuwa tukikemea siku zote, mambo haya yanahitaji kuunganisha nguvu ya pamoja kati ya Serikali, wadau na asasi za kiraia.
Kuna wanafunzi wengi wanawake wananyanyasika vyuoni na maeneo mengine. Kumekuwapo na madai ya kuombwa rushwa ya ngono ili wasaidiwe majibu ya mitihani, jambo ambalo hakika tunaona ni hatari kwa ustawi wa maendeleo ya wanafunzi wetu.
Takwimu zinaonyesha tangu kuanzishwa madawati ya jinsia na watoto vituo vya polisi 420, yamewezesha waathirika 58,059 kuripoti aina mbalimbali za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa rika mbalimbali wakiwemo watu wazima na watoto katika matukio ya ubakaji, ulawiti, vipigo na ukeketaji.
Tunaamini madawati haya yameongeza mwamko mkubwa kwa wananchi kutoa taarifa kwa kujiamini na kusaidia huduma rafiki na kwa haraka kwa wahanga.
Lakini pia tunakubaliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro aliyezindua kampeni wilayani Serengeti mkoani Mara na kusisitiza kuwa eneo hilo limekithiri kwa vitendo hivi na kuitaka jamii ibadilike.
Matukio mengi ya wanawake kukatwa masikio, kupigwa, kuvunjwa mikono na kuachiwa vilema vya kudumu yameshamiri Serengeti, tunasema sasa umefika wakati wa wananchi kubadilika na kuachana na vitendo vya kikatili.
Tunamalizia kwa kuiasa jamii kubadilika na wale wanaotendewa ukatili wa kijinsia kwenda sehemu husika kutoa taarifa kwa wakati.