James Mapalala afariki dunia

0
937

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MWANASIASA mkongwe nchini ambaye pia aliongoza mapambano ya kudai mfumo wa vyama vingi urejeshwe, James Mapalala, amefariki dunia.

Mapalala alifariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Kairuki alikokuwa akitibiwa.

Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Bernard James, alisema baba yao alifariki dunia saa 4:30 asubuhi, akiwa anatibiwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

“Ni kweli baba amefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu, kwani tangu wiki zilizopita alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kupumua, ambapo alikuwa akipata matibabu na baadaye tukampeleka Hospitali ya Kairuki ambako alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu,” alisema James.

Alisema taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu Kinondoni , Dar es Salaam.

Mapalala aliyezaliwa Februari Mosi, 1936 ameacha mke na watoto kadhaa.

Alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza waliojitosa kudai mfumo wa vyama vingi urejeshwe nchini.

Kutokana na madai hayo, Mapalala alifungwa miaka miwili mkoani Lindi kuanzia mwaka 1986 hadi 1989 na baada ya kutoka aliwekwa kizuizini kwa kipindi cha mwaka mmoja katika kisiwa cha Mafia baada ya kuanzisha chama cha siasa wakati sheria ilikuwa hairuhusu.

Alianzisha Chama cha Wananchi (CCW) mwaka 1991 na baadaye kiliungana na chama cha Zanzibar – Kamahuru na mwaka 1993 kuzaliwa Chama cha Wananchi (CUF).

CUF kilikuwa ni chama pekee cha upinzani kilichoweza kujigamba wakati kinazaliwa, kuwa cha kitaifa kimwonekano wake kutokana na matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kilikuwa ni muungano baina ya vyama viwili – Chama cha Wananchi kilichoasisiwa na Mapalala kwa upande wa Bara, na Kamati ya Kupigania Uhuru (Kamahuru) cha Shaaban Khamis Mloo kwa upande wa Zanzibar ambacho baadaye kilikuwa chama cha siasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here