27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JAMBO USILOPENDA MWANAO ATENDE, USILIFANYE MBELE YAKE

Na Christian Bwaya


MAJUZI nilikuwa nawasiliana na mdogo wangu nikiwa nyumbani. Katika mazungumzo yetu hayo, tulijikuta tukitofautiana naye kwa jambo nililoamini hakulifanya kwa usahihi. Hata hivyo, mwishoni tulielewana na tukaagana.

Sikujua kuwa mwanangu aliyekuwa anaendelea na shughuli zake karibu na mimi alikuwa akifuatilia mazungumzo hayo. Baada ya mazungumzo ya simu, mwanangu wa kwanza wa miaka saba akanipokea kwa swali: “Kwanini unamkemea mdogo wako?” Sikutarajia swali kama hilo. Nilishangaa kidogo. Nikamuuliza ufafanuzi akanijibu: “Sio vizuri kumkemea mdogo wako hata kama amekosea.”

Nilikuwa nimepatikana. Kile nilichokuwa namkumbusha mwanangu mara kwa mara kilikuwa kimenirudia. Kwamba nilimfundisha asigombane na mdogo wake, maana yake na mimi sikupaswa kutofautiana na mdogo wangu.

Kisa hicho kilinikumbusha jambo nililokuwa nalifahamu kabla. Kwamba mtoto anajifunza kupitia yale tunayoyafanya kama wazazi kuliko maneno na mafundisho yetu. Mwanangu, kwa mfano, alishangaa kuona ninafanya kinyume na mafundisho yangu. Tabia niliyokuwa nimeionesha ilikuwa na nguvu zaidi ya maneno mengi niliyokuwa nimemwambia kabla.

Tofauti ya maneno na tabia yangu ilimfanya ashindwe kuelewa. Je, achukue tabia niliyokuwa nimeionesha au maneno niliyokuwa nimemwambia? Kipi kilikuwa sahihi zaidi, mafundisho mazuri au tabia iliyokuwa kinyume na mafundisho yangu?

Inawezekana mwanao hajawahi kukuambia wazi wazi lakini huenda anachanganyikiwa kama ilivyokuwa kwa mwanangu. Kile unachokisema, sicho unachokiishi. Huenda hana ujasiri wa kukuambia lakini haelewi kwanini unatarajia awe kinyume na maisha anayoona unayaishi.

Pengine umemwambia mara kwa mara umuhimu wa kusoma kwa bidii, lakini hajawahi kukuona ukisoma. Ukirudi nyumbani unaangalia televisheni hadi unapokwenda kulala lakini huachi kumkumbusha kusoma vitabu na kufanya kazi za shule anazotakiwa kuzinfanya nyumbani. Pengine unazungumza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, lakini anachokiona kwako ni uvivu. Kila kazi unaagiza dada wa kazi afanye na wewe uko ‘bize’ na simu. Anapokutazama, anachanganyikiwa una maana gani unapomfundisha kufanya kazi kwa bidii.

Inawezekana unamkumbusha kila siku umuhimu wa kuwa mtu wa imani, kwenda kanisani/msikitini, lakini hajawahi kukuona ukichukulia masuala ya imani kwa uzito unaostahili. Huenda wewe ni baba unayeipeleka familia yako kanisani/msikitini lakini wewe mwenyewe huingii. Huenda wewe ni baba mwenye michepuko lakini unawakumbusha watoto umuhimu wa kuishi maisha safi ya ujana. Wakikutazama wanashindwa kuelewa: je, wachukue unachokisema au kile wanachokiona unakifanya?

Naomba nikukumbushe kuwa kuna wakati mwanao ataondoka nyumbani na ataenda kuanza maisha ya kujitegemea. Hebu nikuulize, ungependa wakati huo mwanao anapoondoka nyumbani kwako awe mtu wa namna gani?

Jiulize, wakati mwanao anaanza maisha ya ndoa, ungependa mwenzi wake aone tabia zipi kwake? Kama ni ajira, ungetamani awe na sifa zipi zitakazomsaidia kufanya vizuri kazini? Ungependa aishi namna gani na watu?

Wazazi wengi hutamani watoto wao wawe watu wazima  wanaojiheshimu na kuheshimu wengine, wawe waaminifu, wenye uadilifu, uwajibikaji na bidii ya kazi. Najua hakuna mzazi asiyependa mwanawe awe na moyo wa kiasi na nidhamu, ushirikiano na watu, ujasiri, uvumilivu na uwezo wa kutatua changamoto za kimaisha.

Swali la kujiuliza, hata hivyo, ni kwamba sisi wenyewe tunazo tabia hizo? Tunapowafundisha watoto wetu kuwa waaminifu, tunaweza kweli kusema watoto wetu wanaweza kuuona uaminifu huo kupitia maisha yetu ya kila siku? Ni muhimu uwe vile unavyotaka mtoto wako awe.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles