31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Warioba: Bunge lisitishwe

Jaji Joseph Warioba
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba

WAANDISHI WETU, DAR NA DODOMA

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema ni vyema Bunge Maalumu la Katiba likasitishwa kwani Katiba bora haiwezi kupatikana kwa muda wa wiki mbili.

Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja siku moja baada ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kumtaka Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kulisitisha, huku mwenyewe akisema litaendelea na hadi kufikia Oktoba 4 Katiba inayopendekezwa itapatikana.

Jaji Warioba alieleza kushangazwa kwa haraka waliyokuwanayo wajumbe wa Bunge hilo wakati wanajua kuwa Katiba haiwezi kupatikana kwa muda uliobaki.

Alisema wiki mbili au tatu zilizobaki ni chache mno na kwamba Katiba mpya haiwezi kupatikana, hivyo ni vyema sasa busara ikatumika kulisitisha.

“Mimi sizungumzii kauli ya Ukawa, lakini natoa maoni yangu kwamba sidhani kama watamaliza kwa kipindi hiki kifupi, kuna mambo hawawezi kupata kwa muda huu mfupi.

“Ninachotaka watumie tu busara waliahirishe… sijui haraka yao hii ni ya nini. Kwanini wanashindwa kuelewa kuwa Katiba ni suala la maridhiano?” alihoji Jaji Warioba.

Kwa upande wake, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Augustino Ramadhani, alikataa kuzungumzia chochote juu ya suala hilo, akisema tangu Rais Jakaya Kikwete alizindue Bunge hilo, alijitoa kuzungumzia suala la Katiba.

“Kama umefuatilia nilishajitoa tangu siku Rais Kikwete anazindua Bunge la Katiba, nilijitoa kabisa, sitaki kabisa kuzungumzia Katiba tena,” alisema Jaji Ramadhani.

Alipotakiwa kueleza sababu za yeye kujitoa kuzungumzia Katiba, alisema: “Ni uamuzi wangu.”

CHEYO NA UKAWA

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD),  John Cheyo, alisema Bunge hilo haliwezi kusitishwa wala kuongozwa kwa matakwa ya watu waliopo barabarani.

Akizungumza wakati akichangia majadiliano ya jumla ya mchakato wa Katiba mpya, alisema makubaliano yaliyofikiwa baina ya TCD na Rais Kikwete, ni kuhakikisha Bunge hilo linapata Katiba mpya iliyopendekezwa na wananchi.

Cheyo alisema kuwa Bunge hilo linaendelea na kazi yake kwa mujibu wa sheria.

Alisema maandamano yanayotarajiwa kufanywa na vijana wa vyama vinavyounda Ukawa, hayatasaidia lolote.

Alielezwa kushangazwa kwake na matamko ya Ukawa na kueleza kuwa ukweli wa kile kilichojadiliwa upo kwenye video ambayo inaonyesha kila mmoja alivyochangia majadiliano hayo.

“Katiba itakayodumu ni ile ya maridhiano, lakini katika maridhiano haina maana kwamba wanaokaa kuzungumza lazima wang’ang’anie upande wao.

“Wanaokaa kuzungumza maana yake wanatafuta ni vitu gani ambavyo wanaweza kuvizungumza, na ni vitu gani ambavyo vinaweza hata kuwekwa pembeni kwa sasa, lakini baadaye vikaja kushughulikiwa kwa mazingira ya wakati huo, hili tumejifunza tulipokuwa tunazungumza na Mheshimiwa Rais juu ya mchakato wa Katiba na Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Mheshimiwa Rais amekuwa ni mfano mzuri wa kukubali kushauriana, na kama Katiba tunavyoizungumza hapaswi hata kukubali, lakini amejiweka chini akakaa kitako na viongozi wa TCD na viongozi wanaojiita Ukawa,” alisema Cheyo.

Aliongeza kuwa katika mkutano wa kwanza uliochukua muda wa saa nne, majadiliano yalikuwa ni namna gani Katiba itapatikana na Uchaguzi Mkuu utafanyikaje na si vinginevyo.

Moja ya mambo yaliyokubalika ni Bunge la Katiba lipate Katiba inayopendekezwa na wananchi kama ilivyokusudiwa.

“Pia tulikubaliana kwa hali halisi ya muda tulionao haiwezekani mchakato mzima ukamalizika, na maana ya kumalizika mchakato ni kura ya maoni ya wananchi na ndio wenye Katiba,” alisema.

Cheyo alisema katika makubaliano hayo, viongozi wote waliafikiana kuwa awamu ya Bunge Maalumu imalize kazi yake kama ilivyokuwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Bunge hili haliendeshwi kwa amri ya mtu aliyepo barabarani, linaendeshwa kwa mujibu wa sheria ambayo inasema uhai wa Bunge ni Oktoba 4, mwaka huu, wote tulikubaliana,” alisisitiza Cheyo.

Alisema si rahisi Rais akurupuke na kuliahirisha Bunge hilo kwa shinikizo lolote kwa sababu sheria imeweka wazi ukomo wake.

Aliwataka viongozi wa Ukawa kukubaliana na tamko alilolitoa mbele ya vyombo vya habari, ambalo lilipatikana baada ya makubaliano.

Aidha aliwataka wajumbe wenzake kujiamini na kwamba ripoti itakayotolewa na Kamati ya Uandishi ndiyo itakuwa Katiba inayopendekezwa.

“Na kwa sababu yoyote ile, huko nje kuna anayeamini vingine, anaweza kuamini Serikali tatu, na haipo, mimi sitaki, anaamini Kadhi na haipo hiyo ni shauri yako…,” alisema Cheyo.

TEC YAWASHANGAA UKAWA

Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine Niwemugizi, alisema Ukawa walikuwa na kikao cha maridhiano na Rais Kikwete, hivyo walikuwa na nafasi ya kumtaka asitishe Bunge.

Alisema badala yake walitoka kwenye kikao hicho na kuanza kulalamikia wananchi huku wakiwaambia waandamane ikiwa Rais Kikwete atashindwa kusitisha shughuli hizo.

“Inashangaza kuona Ukawa wanalalamika nje ya kikao wakati walikuwa na nafasi kubwa ya kumwambia Rais Kikwete asitishe Bunge mara baada ya kumalizika kwa kikao chao, badala yake wameamua kuja kwa wananchi na kuanza kulalamika.

“Kwani katika hicho kikao hawakuwa na makubaliano? Na kama ni hivyo kwanini walikubali kutumia Katiba ya mwaka 1977 kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani?” alihoji.

Alisema katika kikao hicho Ukawa na Rais Kikwete waliingia makubaliano ya kusitisha mchakato wa Bunge hadi mwaka 2016 ikiwa Rais ajaye atakubali kuendelea nao.

“Nimewashangaa sana wajumbe wa Ukawa, kwa sababu walikuwa na nafasi kubwa ya kuwasilisha malalamiko yao kwa Rais na kuingia makubaliano ya kusitishwa kwa shughuli hizo, lakini baada ya hapo wanakuja kwa wananchi na kuanza kulalamika huku wakidai kuitisha maandamano, kwani hawakuwa na nafasi ya kumwambia rais malalamiko yao,” alisema.

MBOWE

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema hakuna sababu ya kuharakisha mchakato huo na kuwa hata ikibidi baada ya miaka 100, Katiba bora itapatikana.

Alisema jambo muhimu ni Katiba kukidhi mahitaji ya Watanzania na izingatie maoni yao.

“Hatuwezi kuvumilia kuona uchakachuaji wa fedha, unyanyasaji, na ukatili. Yanayoendelea kwenye Bunge la Katiba ni unyama na wizi,” alisema Mbowe.

Taarifa hii imeandaliwa na Elizabeth Hombo, Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam na na Rachel Mrisho, Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. MH JAJI WARYOBA UMEWASAHAU CCM?
    JAJI Waryoba CCM ya zama zenu siyo CCM ya sasa ambayo imetekwa nyara na mabazazi ambao lengo lao ni kushehenesha matumbo yao na siyo ya wananchi wote.
    Wanachokimbilia BMK ambao wengi wao ni CCM uchaguzi mkuu wa 2015. Hilo haswaaa ndilo linamfanya SITTA agangamale manake kwake URAIS ni ishu ya KUFA NA KUPONA hiyo anajiwekea mazingira ya kuwapiga bao watangaza nia wenzake walioko CCM.
    Lakini juhudi zako zimeonekana na zinashikika

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles