24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI WA ESCROW AJIUZULU

Na Bakari Kimwanga-DAR ES SALAAM

WAKATI vinara wa suala la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow wakifikishwa mahakamani kujibu tuhuma  mbalimbali zikiwamo za uhujumu uchumi, Rais Dk. John Magufuli, ameridhia kujiuzulu kwa Jaji  Profesa John Ruhangisa.

Jaji Ruhangisa ni mmoja ya vigogo wa mahakama nchini ambaye alipewa Sh milioni 404.2 kupitia Benki ya Mkombizi, na Mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd,  James Rugemalira.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema Rais Dk. John Magufuli ameridhia maombi ya kustaafu mapema kwa Jaji    Ruhangisa.

Taarifa hiyo ilimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ikisema  a Rais Magufuli ameridhia maombi ya kustaafu mapema kwa Jaji Prof. John Ruhangisa kuanzia jana, Julai 6  mwaka huu.

“Mhe Prof. John Eudes Ruhangisa alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya  Tanzania Kanda ya Shinyanga,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu ingawa haikueleza sababu za kustaafu kwake mapema.

Jaji Profesa Ruhangisa aliapishwa Agosti 15, 2014 na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Jaji wa Mahakama Kuu akiwa na majaji wenzake 19.

Taarifa zaidi ziliiambia MTANZANIA jana kuwa hatua ya kujiuzulu kwa Jaji Prof. Ruhangisha inatokana na uchunguzi uliofanywa kupitia Tume ya Utumishi wa Mahakama  kuhusu majaji wanaotuhumiwa kupokea mamilioni ya shilingi kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Kwa mujibu wa utaratibu wa tume hiyo, baada ya uchunguzi taarifa hupelekwa kwa Rais ambaye baada ya kupitia mapendekezo ya ripoti ya uchunguzi hutoa uamuzi.

Majaji waliotuhumiwa kuingiziwa fedha hizo za Akaunti ya Tegeta Escrow ni Jaji Profesa  John Eudes Ruhangisa anayedaiwa kuingiziwa Sh milioni 404.25 na Aloysis  Mujulizi  Sh milioni 40.4.

Mwaka jana katika maadhimishi ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika Mnazi Mmoja  Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga, alinukuliwa na gazeti hili  akisema  dawa ya kumaliza mambo ni kuwa wazi.

“Suala la majaji waliohusishwa katika Escrow limeshaletwa katika Tume, lipo na taratibu zinaendelea,” alisema Katanga.

Naye Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Enzeel Mtei  alunukuliwa katika maadhimisho hayo ya Wiki ya Sheria akisema tume hiyo iliundwa na wajumbe sita.

Alisema ilikuwa na jukumu la kumshauri Rais juu ya uteuzi wa Jaji Kiongozi au Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu na kutokuwa na uwezo kwa watendaji hao.

Majukumu mengine ni kuchambua malalamiko dhidi ya majaji hao na kuchukua hatua za utawala dhidi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi au Jaji na hatua zilizoainishwa katika Katiba.

Alisema kwa majaji wanaokwenda kinyume na maadili,   tume   huchunguza madai hayo na kupeleka mapendekezo kwa Rais kwa ajili ya uamuzi.

Juni 19, mwaka huu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) iliwafikisha mahakamani vinara wawili wa suala  hilo ambao ni Mwenyekiti wa Mtendaji IPTL/Pan Africa Power (PAP), Harbinder Sethi Singh na mwenzake wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd,  James Rugemalira.

Vigogo hao walifikishwa   katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi.

Watuhumiwa hao pia wanadaiwa kula njama, kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa udanganyifu na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60  (Sh bilioni 309.5).

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao na Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Walipelekwa rumande hadi Julai 3 kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza wala kutoa dhamana kwa kesi ya uhujumu uchumi.

Ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, mwaka 2011 na Machi 19, 2014 Dar es Salaam, watuhumiwa walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao walidaiwa kuwa kati ya Oktoba 18,  mwaka 2011na Machi 19, 2014   Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma na wakisaidiana na watumishi wa umma, walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la nne, mtuhumiwa Sethi anadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai, alighushi fomu namba 14 ya usajili wa makampuni na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua si kweli.

Sethi anadaiwa kutoa nyaraka hiyo ya usajili wa Kampuni kwa Ofisa Msajili wa Makampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Katika shtaka jingine, washtakiwa wote  walidaiwa kuwa kati ya Novemba 28/29, 2011 na Januari 23, 2014 makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi Tawi St. Joseph, kwa ulaghai, walijipatia kutoka Benji Kuu ya Tanzania  (BOT), Dola za Marekani 22,198,544.60  (zaidi ya Sh bilioni 309.5).

Ilidaiwa  kuwa katika shtaka la kusababisha hasara, washtakiwa hao,  Novemba 29, mwaka 2013 katika Benki ya Stanbic Tawi la  Kinondoni, kwa vitendo vyao, waliisababishia Serikali hasara ya USD 22, 198, 544.60 na Sh bilioni 309.5.

Baada ya kumaliza kusomewa mashtaka yao, Wakili wa utetezi,  Respicius Didas kwa niaba ya mawakili wenzao, aliomba mahakama iwapatie wateja wao dhamana kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhaminika.

Hata hivyo upande wa mashtaka ulipinga vikali hoja hizo na kuiomba mahakama kutupilia mbali maombi ya utetezi ya kuwapatia dhamana washtakiwa hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles