24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Nsekela aeleza changamoto sheria ya matamko

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

KAMISHNA wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Harold Nsekela, amekiri na kusema kuna changamoto ya sheria kutokuonyesha ni lini Sekretarieti inaanza kupokea matamko ya viongozi wa umma.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusiana na hali ya urejeshaji wa matamko ya rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma.

Alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya sheria kutokuonyesha ni lini kiongozi wa umma anatakiwa kurejesha tamko lake, hivyo wengi kujikuta wakileta matamko hayo Desemba 31.

“Lakini jambo la msingi ni kweli sheria haizungumzii ni lini tunaanza kupokea hayo matamko, sheria ina ukakakasi, ‘that’s true’, haijasema toka lini unaanza kurejesha, hakuna, haiko, na hiyo ni ‘problematic’,” alisema Jaji Nsekela.

Alisema kuwa kuchelewesha tamko linaweza likawa sio kosa kwa jinsi ambavyo mhusika atajitetea, huku akitolea mfano kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ambaye alichelewesha tamko lake kwa sababu alikuwa mahabusu na walimwelewa.

“Tarehe 31 nimeikataa na nitaendelea kuikataa kwa sababu mchakato bado unaendelea, ndiyo maana nakusomea sheria hiyo, ‘cut off date’ sio tarehe 31, sasa wewe unataka kunilazimisha kwenda kwenye ‘Interpretation’ ya sheria, sio ndio mwisho, kuna watu hata akichelewa akitoa sababu ya msingi hana kosa,” alisema.

Alipoulizwa ni idadi ya viongozi wangapi kwa ujumla wanatakiwa kurejesha matamko, Jaji Nsekela alisema hiyo si kazi rahisi kwake kujua na yeye hawezi kufahamu kwa sababu kila siku Rais anateua na kubadilisha viongozi.

“Hiyo si kazi rahisi, kwanini nakwambia hivyo, kwanza hata vyeo vyenyewe lini unajua kwamba Rais atabadilisha Baraza la Mawaziri, mawaziri si tunao, hebu nikupe mfano. Kuna cheo kimeongezeka mahakamani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama. Je, huyu ni kiongozi? Je walioko chini yake kama hapa Dodoma sio viongozi?

“‘Structure’ ya vyeo hivi vinabadilika mara kwa mara, kwa hiyo huwezi kuwa na ‘figure’ kwa nafasi ambazo zipo wazi,” alisema Jaji Nsekela.

Alisema kuna viongozi 366 wamerejesha matamko yao wakati wao hawakupaswa kufanya hivyo.

Ametolea mfano waliofanya hivyo kuwa ni wanaokaimu nafasi mbalimbali, maofisa madini wakazi, wakuu wa magereza pamoja na makamanda wa wanyamapori.

Hata hivyo katika hatua hiyo, alisema tayari Sekreterieti imepokea fomu za matamko kutoka kwa viongozi mbalimbali wa kitaifa, wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama isipokuwa Naibu Katibu Mkuu mmoja.

Jaji Nsekela alisema changamoto kubwa ambayo wamekutana nayo ni umbali waliokuwa wameweka katika kanda nane za kukusanya matamko hayo.

Alisema hali hiyo imesababisha hadi sasa hivi kutokuwa na idadi kamili ya watu ambao wamerejesha matamko hayo.

“Tuna kanda nane, mfano Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kulikuwa kuna mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Iringa na Njombe na ofisi zetu hazipo kila mahala, hivyo imekuwa ngumu kupata yote kwa wakati.

“Ila niwahakikishie mpaka sasa siwezi kulalamika tena kwamba hawajarejesha, mwitikio umekuwa mzuri na viongozi wote kitaifa wameleta,” alisema Jaji Nsekela.

Hata hivyo, alipoulizwa kukosekana kwa meno kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ikiwamo kushindwa kuwachukulia hatua wale ambao hawarejeshi matamko, Jaji Nsekela alisema yeye anafanya kazi kwa kufuata Katiba ya nchi.

“Hatujiendeshi tu, tunajiendesha kwa kufuata Katiba, hii hapa soma Katiba ibara 132, ukiisoma vizuri utajua sisi ni nani na tuna meno.

“Ukija kuisoma sheria yetu itakuonyesha sisi tuna meno, lakini inawezekana meno yetu ni ya raba, lakini meno tunayo. Unasema hatuna meno? Meno nitakueleza sasa, kifungu cha nane cha sheria yetu ya adhabu zetu, kuna kuonya na kupewa tahadhari, kushushwa cheo, bado hakuna meno?

“Ukishushwa cheo hata mshahara wako unashuka, bado haina meno? Hiyo sijui, kusimamishwa kazi bado unaona sawa tu?

“Kwa mawaziri na wabunge wanapoteza sifa kama hawatotoa tamko, huko sitaki kwenda kwa sababu nikienda huko kuna wahusika, unapoteza ‘qualification’ (sifa) ya kugombea cheo chako, kama waziri hajarejesha, asipoleta, ndiyo maana unaona mawaziri wote wameleta,” alisema.

Alipoulizwa anakutana na changamoto gani katika utendaji kazi wake, Jaji Nsekela alisema aliyemteu ndiye anatakiwa ajue anakutana na changamoto gani na si mtu mwingine.

“Aliyenipa hiki cheo ndiye anajua changamoto zake, mimi siwezi kumwambia kuna changamoto, amenipa amesema nikasome katiba na sheria na ninaitekeleza ya kuniambia nitafute kazi sio mimi, ngojeni mwingine, kila mmoja amepewa kazi yake, mimi nimepewa kazi ya maadili,” alisema Jaji Nsekela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles