Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM
MSAJILI wa Vyama Vya Siasa, Jaji Fransic Mutungi, amevionya Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Amevitaka kuacha mara moja kutishana au kuchukua sheria mkononi kutokana na malumbano yanayoendelea ndani ya vyama hivyo.
Ametoa kauli hiyo siku chache baada ya Chadema kudaiwa kuingilia mgogoro wa ndani wa Chama cha Wananchi (CUF) na kuwatishia wanachama wa chama hicho waliokua matawini, hali iliyosababisha CUF kutangaza kupambana jino kwa jino juzi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Jaji Mutungi, alisema licha ya vyama hivyo kutishana, hakuna hata chama kimoja kilichowasilisha barua ya malalamiko kwenye ofisi yake kutokana na madai yao.
Alisema kinachotokea sasa ndani ya vyama hivyo ni kutishana huku wakijua kuwa siku ya kufanya uamuzi wa vitisho hatua za sheria zitachukuliwa dhidi yao.
Mutungi alisema vyama vyote vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na hakuna chama kinachofanya kazi kwa matakwa yake, hivyo chama kitakachoamua kuvunja sheria kwa makusudi kitachukuliwa hatua kali.
“Natoa onyo kwa chama chochote cha siasa ambacho kitaonyesha ubabe na kutumia wafuasi wake waweze kufanya vurugu.
“Tutakichukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria, lakini pia mtu atakayekubali kutumwa kwa ajili ya kufanya vurugu na yeye atachukulia hatua kali,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema viongozi wa vyama hivyo waendelee kutishana lakini itakapofika wakati wa kufanyiana vurugu hakuna atakayesalimika, lazima watachukuliwa hatua.
“Kama kungekua na tatizo wangeleta barua ofisini kwangu ya malalamiko, lakini mpaka sasa sijapata barua yoyote inayohusiana na madai yao zaidi ya kusoma kwenye vyombo vya habari.
“Hivyo basi watakaopigana kwa ajili ya vyama vyao tutawawajibisha kisheria,” alisema.
Alisema mkakati wa ofisi yake ni kuendelea kuwaelimisha wanasiasa waweze kufanya shughuli zao kwa ustaarabu, hali itakayowasaidia kuongeza wafuasi kuliko kuendeleza migogoro isiyo na tija.
Ndoa ya CHADEMA na CUF (UKAWA)ndilo tatizo. Chadema wanadhani CUF ya Lipumba sio ile waliyofunga nayo ndoa na hivyo kutaka kuitia adabu.
Nisichofahamu ni uhalali wa CHADEMA kutisha CUF ya Lipumba.
Ngoja tusubiri kuona mwisho wa wanaume hawa ambao wanadhani uhuru wao hauna mipaka!