27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Jaji Mkuu awaasa majaji wapya

ANDREW MSECHU – dar es salaam

JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amewataka majaji kusahau mazingira ya kazi waliyotokea kabla ya uteuzi na kuwataka kuwa tayari kukabiliana na mazingira mapya, ambayo hayahitaji usaidizi zaidi ya uwajibikaji binafsi.

Akizungumza katika hafla ya kuapishwa kwa majaji wapya 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani, Ikulu Dar es Salaam jana, Profesa Juma aliwataka kutambua kuwa jaji ni mtu asiyelala, hana mwisho wa wiki wala sherehe, bali siku zote yuko kazini na akiwa kazini hana msaidizi, ni yeye na jalada lake tu.

“Kwa majaji mlioteuliwa muwe tayari kufanya kazi katika sehemu yoyote mtakayopangiwa nchini. Na katika hili tukitoka hapa tusianze kutafutana kuwa nani anabaki Dar es Salaam.

“Kwa wale ambao mnatoka katika maeneo ya kazi ambayo yalikuwa na wasaidizi kadhaa, ambao mlikuwa mkitekeleza majukumu kwa kutoa maelekezo au kuagiza, mjiandae kwa mazingira mapya ya kazi.

“Mtambue kuwa jaji anafanya kazi mwenyewe kwa saa 24, anabeba mafaili yake mwenyewe mahakamani na hata kwenda nyumbani kwake. Hana sikukuu wala mwisho wa wiki,” alisema.

Alisema kwa majaji wa karne ya 21 wana changamoto nyingi, hivyo ni vizuri kwa huu muda mchache watakaokwenda kukabidhi ofisi waanze kujiandaa kwa maisha mapya.

“Elimu endelevu ni muhimu, zamani tulikuwa tunaambiwa jaji anajua kila kitu, lakini hapa baada ya kiapo mtakwenda kozi kwa mwezi mmoja, kwa sababu mwananchi akikuona mara ya kwanza mahakamani hajui wewe ni jaji mpya anajua wewe ni jaji,” alisema.

Pia aliwataka majaji wapya walioapishwa na kuongeza idadi ya majaji wa Mahakama Kuu kutoka 66 waliokuwepo awali hadi 81 kuzingatia sheria na kufanya haki katika kutoa uamuzi bila kujali hali ya mtu.

Aidha, aliwataka kujiepusha na vishawishi na rushwa kwa kuwa wanategemea malipo kutoka sehemu moja tu ambayo ni Serikali na iwapo kutakuwa na chanzo kingine cha kipato basi iwe ni biashara halali ili kuepuka mgongano wa kimasilahi utakaosababisha watu wengine wasipate haki.

“Kama jaji ana bodaboda na ikakamatwa ukampigia Afande Sirro (Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro) ili isiende mahakamani hiyo haikubaliki,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, Profesa Juma alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa idadi kubwa ya majaji na kuongeza kuwa itasaidia kupunguza mzigo wa kesi anazosikiliza jaji mmoja.

“Uliniuliza unataka majaji wangapi, nikakwambia una majina 60 mezani kwako. Nashukuru ulipopata takwimu zetu wewe ulikuwa wa kwanza kunikumbusha hali ya majaji Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani si nzuri.

“Nawapongeza majaji wapya, nimesikiliza viapo vyenu kuonesha utayari kwenda kutumikia jamhuri, tusianze baada ya hapa kuulizana nani anataka kubaki Dar es Salaam, utakuwa umekiuka masharti ya kiapo chako,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Sheria Profesa Paramagamba Kabudi alisema suala muhimu kwa sasa ni kuhakikisha kunakuwepo ‘mahakama zinazotembea’ ili kurahisisha huduma za mahakama kwa wananchi wengi zaidi.

Alisema kukamilika kwa mpango huo kutasaidia kupunguza mzigo kwa kuwafikia wananchi wengi katika maeneo yasiyokuwa na majengo au miundombinu ya mahakana na kurahisisha utaratibu wa upatikanaji wa haki.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,573FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles