25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu atoa ushauri kumaliza mimba za utotoni

Gurian Adolf-Sumbawanga

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, ameutaka uongozi wa Mkoa wa Rukwa kutotegemea sheria pekee kumaliza tatizo la mimba za utotoni, badala yake jamii ihusishwe katika kutafuta suluhu ya changamoto hiyo.

Hayo aliyasema jana alipokuwa akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Rukwa wakati wa ziara yake ya siku mbili kutembelea na kukagua utendaji wa mahakama katika wilaya za mkoa huo.

Alisema suala la mimba za utotoni inabidi kuishirikisha jamii moja kwa moja ili kuzungumza kwa lugha moja na kuja na suluhu ya changamoto hiyo na si kutegemea sheria pekee ndio zitamaliza tatizo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachimu Wangabo alisema katika mwaka huu mkoa una mimba za utotoni 294, ambapo tayari kuna mpango mkakati umeandaliwa utakaoshirikisha wadau wote katika kudhibiti changamoto hiyo.

Alisema hivi karibuni kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kitaketi na moja ya ajenda itakuwa ni kujadili mikakati ya namna ya kukabiliana na tatizo hilo sugu, na utekelezaji wake utaanza mara moja.

Katika hatua nyingine, Profesa Juma alisema mahakama inaangalia uwezekano wa kuanza utaratibu wa kutoa nakala za hukumu kwa lugha ya Kiswahili ili kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa haki katika vyombo vyake vya maamuzi.

Alisema hoja ya mahakama kutoa nakala za hukumu kwa lugha ya Kiswahili ni jambo la msingi na litasaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki kuhusu mashauri mbalimbali.

Profesa Juma alisema pia itawasaidia kufahamu na kuelewa kwa urahisi kile kilichoamuliwa na mahakama, hivyo yule anayetaka kukata rufaa mahakama ya juu inakuwa rahisi kwake kufanya hivyo na kwa wakati sahihi.

“Hii hoja ya kutumia lugha ya Kiswahili katika mahakama zetu ni jambo la msingi na muhimu sana. Tumeipokea na tutaifanyia kazi,” alisema

Hoja hiyo, iliibuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Halfan Haule ambaye alisema wanaiomba mahakama kuona umuhimu wa kutoa nakala za hukumu kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi wawe na uelewa wa kile kilichoamuliwa kuliko ilivyo sasa ambapo wengi wao utembea na nakala ya hukumu kutafuta wakalimani hadi inachakaa.

Alisema hata wale wanaohitaji kukata rufaa baada ya kutoridhishwa na hukumu ya awali, hujikuta wakichelewa kufanya hivyo kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta wakalimani ambao wakati mwingine wanahitaji fedha.

Dk. Haule alisema hali hiyo imesababisha wananchi wengi kupoteza haki zao za msingi kutokana na kutoelewa kile kilichoandikwa katika hukumu iliyotolewa na mahakama husika kwani angefahamu mapema labda angeweza kukata rufaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles