24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MKUU ATAKA WELEDI MAHAKAMA ZA MWANZO

 

Na ABDALLAH AMIRI


JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amewaagiza mahakimu wa mahakama za mwanzo na wilaya nchini kuboresha utendaji wa kazi zao ikiwa ni pamoja na kutenga muda maalumu wa kutoa elimu kwa wananchi waweze kutambua haki zao.

Alikuwa akizungumza jana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Igunga mkoani  Tabora wakati wa ziara yake.

Alisema kazi ya mahakama ina changamoto  nyingi kwa kuwa baadhi ya wananchi hawatambui namna ya kudai haki zao mahakamani.

Jaji mkuu alisema  ni wajibu wa mahakimu kutenga muda maalumu wa kutoa elimu kwa wananchi   waweze kujua haki zao  sheria.

Alisema endapo elimu itaendelea kutolewa kwa wananchi ikiwamo mabango na kukemea vitendo vya rushwa itasaidia kupunguza msongamano wa kesi zisizo za lazima katika mahakama.

Jaji Juma alisema wananchi wanapaswa kutambua haki yoyote inapotafutwa inapaswa kuanzia majumbani mwao kwa kuwa yapo baadhi ya mambo wanaweza kuyasuluhisha pasipo kuyafikisha mahakamani.

Alisema mabaraza ya kata nayo ni mazuri kwa kusimamia utoaji wa haki kwa wananchi.

Profesa Juma alisema  endapo yatawezeshwa na kuelimishwa yatapunguza msongamano wa kesi zisizo za lazima katika mahakama za mwanzo na wilaya.

Vilevile aliwataka  wakuu wa wilaya  nchini kusikiliza matatizo ya wananchi katika maeneo yao na kuyapatia ufumbuzi.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya alisema  wilaya hiyo ina wakazi wapatao 420,933 ikiwa ni  ongezeko la wastani wa asilimia 2.9 kwa mwaka.

Alisema kutokana na idadi kubwa ya wananchi inahitajika huduma za  mahakama ikizingatiwa wilaya ina mahakama za mwanzo 10 na mahakama moja ya wilaya wakati ina  tarafa nne, kata 35 na vijiji 119.

Mwaipopo alisema kutokana na hali hiyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma za mahakama.

Alimwomba jaji mkuu kujengwa mahakama za mwanzo katika kata zote 35 na endapo uwezekano huo hautakuwapo angalau ziwepo mahakama 15 za mwanzo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles