25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu ataka DNA itumike kesi za ubakaji

Elizabeth Kilindi -Njombe

JAJI Mkuu Profesa Ibrahim Juma amesema ili kubaini na kuwatia hatiani watuhumiwa wa ubakaji na kufanikisha ushahidi wa wafanyaji vitendo hivyo, kunapaswa kuwapo upimaji wa vinasaba (DNA).

Akizungumza mkoani hapa jana, akiwa katika ziara ya siku tatu ya kukagua mahakama na miradi ya mahakama, Jaji Juma alisema mahakama inafanya mkakati wa kuzifanyia kazi kesi kubwa, zikiwamo za mauaji na ubakaji ili kupunguza msongamano wa mashauri.

“Kuna kesi za mauaji, kubaka, kulawiti watoto… hapa Tanzania tumekuwa na sheria ya DNA tangu mwaka 2009, teknolojia hii itarahisisha badala ya kumwacha mtoto anapofika mahakamani aanze kuhojiwa, aanze kubabaishwa na maswali, kipimo hiki kitasaidia,” alisema Jaji Juma.

Alisema bahati mbaya haoni matumizi ya vifaa hivyo ipasavyo na kutaka uwepo usambazaji wa vipimo kwa wingi katika vituo vya polisi na hospitalini.

“Wataalamu wanasema vipimo vya DNA ukinunua kwa wingi, ghala la dawa wakiweza wananunua na kuleta vituo vya polisi na hospitali, tunaweza kupata vipimo na vikatumika kusaidia kutatua baadhi ya hizi kesi,” alisema.

Alisema mara nyingi mshtakiwa amekuwa akiachiwa kutokana na mahakama kuangalia ushahidi tu.

“Wakati mwingine mashahidi wakianza kubabaika, mahakama huwa inapata shida, pengine mtuhumiwa alistahili kutiwa hatiani, lakini ushahidi unakosa uzito,” alisema Jaji Juma.

Alisema ziara yake mkoani hapa ni mahususi kushiriki kikao cha Mahakama ya Rufani ambacho kilianza kuketi Agosti 12 hadi 30, mwaka huu kikijumuisha majaji wanne ambao wanasikiliza rufani 24 za jinai kutoka Kanda ya Iringa na Mbeya, madai mbili, ombi moja la madai na maombi mawili ya jinai.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka, akizungumzia ujio wa Jaji Juma, alisema anaamini changamoto zilizopo za mlundikano wa kesi za mauaji magerezani zitatatuliwa.

Alisema hadi sasa watuhumiwa wa makosa ya mauaji wapo 156 na makosa ya uhujumu uchumi nane.

Ole Sendeka alisema uwapo wa mahakama kuu, kutasaidia kupunguza safari za majaji wanaosikiliza kesi za mauaji kusafiri kutoka Mahakama Kuu ya Kanda Iringa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles