27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu aagiza kupelekewa mashauri ya mirathi nchi nzima

Na LYDIA CHURI – MTWARA

JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Juma ameagiza kupelekewa mashauri yote ya mirathi nchi nzima ili aweze kujua ni changamoto gani inayofanya yachelewe kumalizika na kupanga mkakati wa kisheria ili yawe yanaisha ndani ya muda uliowekwa.

Akizungumza katika ziara yake ya kikazi aliyoanza juzi mkoani hapa, Profesa Juma alisema katika mahakama za mwanzo mashauri hayo yanatakiwa kuisha ndani ya miezi sita, lakini yapo mengine yamekaa zaidi ya miaka kumi.

“Kutokana na kuchelewa kumalizika kwa mashauri hayo, wakati mwingine humfanya msimamizi wa mirathi kuendelea kunufaika na mali za marehemu wakati warithi wapo na wanataabika kwa muda mrefu,” alisema.

Profesa Juma alisema kuwa ametoa agizo hilo pia kwa kuwa mashauri ya aina hiyo huweza kuzalisha migogoro mingi katika jamii na kusababisha haki kutopatikana kwa wakati.

Akizungumzia changamoto nyingine zinazoikabili Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza jukumu lake la msingi la utoaji wa haki, Profesa Juma alisema inakabiliwa na changamoto kubwa ya wananchi kutofahamu taratibu za kisheria jambo linalosababisha washindwe kupata haki kwa wakati.

“Hivi sasa Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya taratibu za kisheria kabla ya kesi kuanza kusikilizwa mahakamani ili kuwasaidia kutambua nini cha kufanya.

Kwa mujibu wa Profesa Juma, mahakama imeamua kuwa wazi katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni moja ya hatua muhimu za mapambano dhidi ya rushwa ndani ya mhimili huo.

Awali Profesa Juma akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, aliwaomba wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini kushirikiana na mahakama katika kuwaelimisha wananchi taratibu za mchakato wa upatikanaji wa haki.

“Mahakama inachangia utulivu na amani katika nchi pale inapotekeleza jukumu lake la msingi la utoaji wa haki kwa wakati na endepo haitafanya kazi yake vizuri ni wazi amani itatoweka,” alisema. 

Aliongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 pia imetoa mwelekeo wa amani.

Naye Byakanwa akimkaribisha Profesa Juma ofisini kwake, alisema Serikali kupitia mkoa wake inashirikiana vizuri na mahakama katika kuwahudumia wananchi na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.

Wakati huohuo, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Solanus Nyimbi alisema mhimili huo umeandaa mpango kabambe wa ujenzi uliozingatia maeneo yanayotakiwa kujengwa majengo mapya na yanayotakiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa ili kutatua changamoto ya uchakavu na ukosefu wa miundombinu ya mahakama.

Nyimbi alisema hivi sasa majengo yanayoendelea kujengwa ni pamoja na mahakama za mwanzo 22, mahakama za wilaya 20, mahakama za mikoa (Hakimu Mkazi) nane na Mahakama Kuu mbili, yanayojengwa katika mikoa ya Mara na Kigoma.

Alisema Wilaya ya Tandahimba nayo iko kwenye mpango wa kupatiwa jengo litakalojumuisha mahakama ya wilaya na ya mwanzo. 

Aliongeza kuwa lengo ni kuwa na mahakama katika kila makao makuu ya tarafa.

“Ifikapo mwaka 2021 wilaya zote zisizo na majengo ya mahakama zitakuwa tayari zimepatiwa majengo hayo na ujenzi huo utatumia fedha za ndani pamoja na za Benki ya Dunia,” alisema Nyimbi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles