Aziza Masoud na Mauli Muyenywa, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Chama cha Majaji Wastaafu (Tarja), Jaji Thomas Mihayo, amesema kutokana na mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba ulivyo, chama hicho kilifanya uamuzi wa busara kukataa kupeleka mwakilishi katika Bunge hilo.
Kauli hiyo imetolewa wakati hatima ya kupatikana kwa Katiba mpya ikiwa imegubikwa na hali ya sintofahamu, kutokana na hatua ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vinavyoendelea na shughuli ya kujadili na kupitisha vipengele mbalimbali vya rasimu mjini Dodoma.
Akizungumza katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame (77) aliyefariki Jumatatu ya wiki hii, Jaji Mihayo alisema wakati Serikali ikiwa katika mchakato wa kutafuta wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kwenda katika Bunge Maalumu la Katiba, Wizara ya Katiba na Sheria iliiomba Tarja kutoa mwakilishi lakini walikataa kutokana na sababu mbalimbali.
“Tuliambiwa tuchague mwakilishi na Wizara ya Katiba na Sheria lakini tulikataa, baada ya kusikia yanayotokea Dodoma tuliona uamuzi wetu ulikuwa sahihi maana ingekuwa aibu kwetu pia,” alisema Jaji Mihayo.
Akimzungumzia marehemu Makame, Jaji Mihayo alisema alimfahamu muda mrefu akiwa kama jaji mzoefu katika kundi la majaji nchini.
Alisema kupitia Jaji Makame alijifunza vitu vingi ikiwemo uandishi na uamuzi mzuri wa hukumu za kesi mbalimbali kubwa na ndogo.
“Jaji Makame alikuwa mtu wa kujishusha, taa imezimika tulikuwa tukimtegemea kwa vitu vingi, moja ya mtu ambaye anasifika kwa Kiingereza kizuri hasa katika uandishi wa hukumu, alikuwa ana uwezo wa kuandika hukumu ya karatasi tatu kwa aya moja tu na ikaeleweka,” alisema Jaji Mihayo katika shughuli hiyo ya kuaga mwili wa Jaji Makame iliyoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kwa upande wa Jaji Mkuu, Othman Chande alisema Jaji Makame akiwa kama kiongozi na mwanzilishi wa shughuli za mahakama nchini, alikuwa akifanya kazi hiyo kama sehemu ya maisha yake.
“Heshima ni kumuenzi kwa kumuheshimu kama mwanasheria, Jaji, mwanataaluma na wadhifa huo alikuwa nao kwa kipindi cha miaka 42, sheria kwake ilikuwa sio ajira bali ulikuwa mwenendo wa maisha yake, alikuwa na kipaji cha kuchambua masuala ya kisheria,” alisema Jaji Othman.
Alisema Jaji Makame ni miongoni mwa majaji wa kwanza walioteuliwa na Rais wa kwanza nchini, Julius Nyerere na alianza kutumikia cheo hicho akiwa na miaka 32.
Alisema enzi za uhai wake moja ya vitu ambavyo alikuwa anasisitiza ni kuhimiza kutoa haki kwa wakati unaotakiwa.
“Wakati akiwa bado Jaji wa Mahakama Kuu aliwahi kupelekewa zawadi za chupa mbili za mvinyo nyumbani kwake siku ya sikukuu alizikataa kwa maandishi na kusisitiza kwamba hanunuliwi.
Huu ni mfano mzuri wa kiongozi, watu wengi wanashindwa kuchora mstari baina ya matakwa ya maadili na vizawadi zawadi,” alisema Jaji Othman.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini (NEC), Jaji Damian Lubuva ambaye alipokea kijiti cha uongozi kutoka kwa Jaji Makame, alimuelezea mtangulizi wake huyo kuwa mwenye rekodi kubwa ndani na nje ya nchi hasa kwa kusimamia chaguzi nne zilizokuwa katika kipindi kigumu cha siasa.
“Ameweka historia kubwa, ndani ya NEC alikaa miaka 15 na kusimamia uchaguzi wa mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010, mambo mengi aliyafanyia mabadiliko, sisi tulikuwa tunamtumia kama dictionary (kamusi) yetu ya mfukoni, amenisaidia sana kunifariji katika changamoto nilizokuwa nikikutana nazo wakati wa uchaguzi,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa hospitalini wakati akiwa amelazwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa mwisho na alimkuta akiwa amechangamka na kuonyesha sura ya matumaini.
Jaji Makame ambaye anazikwa leo kijijini kwao Tongwe, Muheza Tanga alizaliwa mwaka 1937 na kabla mauti hayajamfika alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya tumbo yaliyosababisha kufanyiwa upasuaji mara tatu.
Shughuli za kuuaga mwili wake zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakuu, wastaafu, wanasheria, majaji na watu wa kada mbalimbali.
Baadhi waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye.
Wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, Profesa Abdallah Safari na Profesa Mwesiga Baregu.
Mwili wa Jaji Makame ulisafirishwa jana baada ya misa ya kumuombea iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Albano, marehemu ameacha mjane, watoto, wajukuu na vitukuu.