23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Jaji Makame afariki dunia

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Lewis Makame.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Lewis Makame.

NA WAANDISHI WETU

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Lewis Makame, amefariki dunia.

Taarifa ambazo MTANZANIA ilizipata zinaeleza Jaji Makame alifariki dunia jana katika Hospitali ya AMI Trauma Center, iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam alipokuwa akitibiwa.

Baada ya kupatikana kwa taarifa hizo, MTANZANIA lilifika nyumbani kwa marehemu Masaki ambako mmoja wa watoto wa marehemu aliwafukuza waandishi wa habari huku akitoa sharti kwa chombo kinachotaka kuripoti msiba wa baba yake, lazima kiwe na kibali cha Serikali.

Mtoto huyo wa marehemu baada ya kutoa kauli hiyo, aliwaamuru wanahabari kutoka nje ya nyumba hiyo na familia haiko tayari kuwaona wakati wote wa maandalizi ya mazishi ya Jaji Makame.

“Hatutaki muingie ndani wala kurekodi habari yoyote kwenye msiba wetu, kama mnataka nendeni mkatafute kibali kutoka serikalini ili mje kuripoti.

“Kama mnasema baba alikuwa mtu wa Serikali nendeni mkawaambie wawape kibali, lakini sisi hatutaki muingie ndani,” alisema mtoto huyo.

Baada ya kusema hivyo, waandishi walimuuliza kama kwenye misiba kunatolewa kibali cha kuripoti matukio na akajibu: “Nimesema sitaki kumuona mwandishi yeyote kuingia ndani.”

Kitendo hicho kiliibua malumbano makali kati ya mtoto huyo wa marehemu ambaye alitaka kuvunja kamera za wanahabari ili wasiweze kurekodi tukio hilo la msiba.

“Nimesema hatutaki waandishi kuingia ndani, nitavunja kamera yenu, ondokeni, hamsikii?” alifoka.

Hata hivyo, MTANZANIA lilipowasiliana na Idara ya Habari (Maelezo), ilithibitisha kutokea kwa msiba huo huku wakisema familia ya marehemu ndiyo itatoa taarifa kamili kuhusu taratibu za mazishi.

“Ni kweli tumeongea na Mkurugenzi wa NEC, Julius Malllab, lakini yupo nchini Afrika Kusini kikazi ila amethibitisha kutokea kwa msiba huu. Lakini sisi kwetu tunasubiri kauli ya familia,” alisema mmoja wa wakurugenzi wa Maelezo.

Jaji Makame alikuwa Mwenyekiti wa NEC na aliiongoza kwa miaka 17 kuanzia mwaka 1994 hadi alipostaafu  2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Jaji Damian Lubuva.

Akiwa Mwenyekiti wa NEC, alifanikiwa kusimamia chaguzi zote zilizofanyika tangu uliporuhusiwa mfumo wa vyama vingi. Kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 1995.

Mbatia amlilia

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema kifo cha aliyekuwa Jaji Makame ni pengo kubwa hasa kwa wanasiasa na wanataaluma wa sheria nchini.

Akizungumza na MTANZANIA, Mbatia alisema Jaji Makame alikuwa mmoja wa viongozi waliosaidia kuimarisha nguvu ya vyama vya siasa, hasa upinzani kwakuwa alikuwa na sifa ya usikivu na kuwa msimamo katika uamuzi anaotoa.

“Nilimfahamu Jaji Makame mwaka 1994 wakati huo sisi tulikuwa vijana, tukienda kwenye vikao tulikuwa tunamtolea kauli kali, lakini alijitahidi kuwa msikivu, mvumilivu na alikuwa mtu wa kutafakari mambo anayoambiwa na kuyafanyia uamuzi ambao huwezi kuubadilisha akishaamua,” alisema Mbatia.

Alisema katika kipindi cha uongozi wake akiwa kama Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Makame alikuwa si mtu wa lawama na kujibizana na wanasiasa mara kwa mara.

“Kiongozi mwenye sifa ya kusikiliza huwa hana tabia ya kuhamaki, mara nyingi alikuwa anafanya uamuzi mwenyewe, watu wenye sifa hiyo ni wachache sana nchini,” alisema Mbatia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles