Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
ALIYEKUWA Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Kipenka Mussa amestaafu kazi ya utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na gazeti juzi, Jaji Mussa alisema kwa mujibu wa Ibara ya 120(1) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatamka Jaji wa Mahakama ya Rufani kustaafu kazi hiyo akiwa na umri wa miaka 65.
” Disemba 28, ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwangu,pia siku hiyo nilistaafu kazi rasmi….namshukuru Mungu nimestaafu kazi hii ya utumishi wa umma niliyoitumikia kwa muda mrefu salama”.
Mussa kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Rais Jakaya Kikwete alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda mbalimbali ikiwemo Arusha, Tanga, Bukoba.
Jaji Mussa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kuchunguza mauaji ya wafanyabiashara wa madini wa Mahenge . Tume hiyo iliundwa na Rais Kikwete ambayo ilipewa jina la “Tume ya Jaji Kipenka’ ilimhoji aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam ( ACP- Abdallah Zombe na maofisa wengine wa polisi kwa tuhuma za mauaji ya wafanyabiashara hao.
Jaji Mussa aliwahi kuwa Katibu wa Bunge, wakili wa Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Haki za Binadamu ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.