26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Augustino Ramadhani 1945-2020

 MWANDISHI WETU –DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na waumini wa Kanisa la Anglikana kufuatia kifo cha Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani kilichotokea jana asubuhi.

Katika salamu zake kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa jana, Rais Magufuli alisema Jaji Mkuu mstaafu Ramadhani atakumbukwa kwa utumishi uliotukuka kwa nchi yake, ulioshadidishwa na umahiri wake, ukweli, uchapakazi, uzalendo wa kweli na ucha Mungu.

“Nakumbuka nilipokwenda kumuona hospitali, mazungumzo yake yalikuwa ni ya kumtumaini na kumtegemea Mungu, kwa hiyo na mimi namwombea kwa mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, amina,” alisema Rais Magufuli.

Alimpa pole Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma na alimwomba kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya marehemu, majaji, mahakimu na wafanyakazi wote wa mahakama pamoja na waumini wa Kanisa la Anglikana kwa kuondokewa na mpendwa wao. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kuthibitishwa na wanafamilia, Jaji Mkuu mstaafu Ramadhani alifariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan, Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.

MWANAYE AELEZEA KIFO CHAKE

Mtoto wake wa kiume, Yakud Ramadhani jana alielezea kifo cha baba yake huyo na kusema alikuwa anasumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu, ambapo pia hata kabla ya mauti kumfika aliwahi kwenda kutibiwa nchini Kenya.

“Amefariki leo (jana) mida ya saa mbili asubuhi, alikuwa akitibiwa katika Hospitali ya Aga Khan na baadaye akaenda Kenya kwa matibabu zaidi na baadaye akarudi nyumbani, lakini akawa bado anaumwa, sasa hivi wanafamilia wanafanya taratibu, kwa chochote kitakachotokea tutawajuza,” alisema Yakud.

Aidha kwa upande wa taarifa zilizotolewa na Mahakama ya Tanzania zilieleza kuwa Jaji Ramadhani alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Jaji Ramadhani aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania mwaka 2007 hadi mwaka 2010 alipostaafu.

Miongoni mwa nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, wadhifa alioushika kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia 2014 hadi 2016.

Pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete Julai 4, 2012.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles