31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji amwonya wakili kesi ya Mwalle

NA JANETH MUSHI, ARUSHA

JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Gadi Mjemas anayesikiliza kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili Wakili Median Mwalle na wenzake watatu, amemwonya na kumtaka Wakili wa Jamhuri, Pius Hilla, amuulize shahidi wake kuhusu kesi iliyopo mahakamani na si kuuliza juu ya mafunzo.

Jaji Mjemas alitoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati akisikiliza ushahidi wa shahidi wa pili wa Jamhuri, Suleiman Nyakulinga, katika kesi inayoendelea kusikilizwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha.

Katika mahojiano hayo Wakili Hilla, alimtaka shahidi ambaye ni ofisa wa polisi wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya uhalifu wa kifedha, aeleze kuhusu kuhudhuria kwake mafunzo kwenye nchi mbalimbali ikiwamo Botswana.

Hata hivyo, uongozaji huo wa maswali ulionekana kumkera Jaji Mjemas ambaye aliingilia kati mahojiano hayo na kumtaka Wakili Hilla kwenda moja kwa moja kwenye jambo lililopo mahakamani badala ya kuuliza
maswali kuhusu mafunzo aliyoyapata.

Mahojiano kati ya Wakili Hilla na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo.

Wakili Hilla: Hebu ieleze mahakama Agosti, mwaka 2011 ulifanya kazi gani ya upelelezi.

Shahidi: Nilikuwa napeleleza akaunti ya East Africa Malaria and HIV Support Program ambayo ilikuwa imefunguliwa kwa njia ya udanganyifu na
tulibaini mmoja wa watia saini wa akaunti hiyo ni mtia saini kwenye akaunti nyingine ya Moyale Precious Gems and Minerals Enterprises.

Wakili Hilla: Mlibaini nini kuhusu hiyo akaunti?

Shahidi: Tulibaini kwenye vitambulisho vya makazi kulikuwa na majina mawili, hati za kusafiria za uraia wa Marekani zilikuwa na majina mawili lakini zikiwa na namba moja.

Wakili Hilla: Mlibaini nini kingine?

Shahidi: Tulibaini Michael Crispine Chacha wa akaunti ya East Africa kwenye akaunti ya Moyale alijiita Ogembo Mitchell Chacha wakati
picha ilikuwa ni moja katika akaunti zote.

Wakili Hilla: Nini kiliendelea baada ya kuhoji na kukusanya nyaraka za kesi hiyo?

Shahidi: Baada ya uchambuzi wa nyaraka tulizokuwa tumekusanya, tulibaini kulikuwa na kesi zaidi ya moja tuliyokuwa tunafuatilia ambayo ni udanganyifu kuhusu akaunti ya East Africa na kesi inayohusu Moyale

Wakili Hilla: Mlifanya nini baada ya kubaini hivyo?

Shahidi: Niliwasiliana na DCI kwa ushauri na kuagiza ifunguliwe kesi nyingine kuhusu akaunti ya Moyale ambayo ni tofauti na ya malaria tuliyokuwa tunafuatilia.

Wakili Hilla: Nini kiliendelea baada ya maagizo hayo?

Shahidi: Nilihoji washtakiwa wa kesi hii akiwemo Mwalle na Boniface Mwimbwa ambaye alikuwa Meneja wa CRDB, tawi la Meru, Arusha kuhusiana na
akaunti ya Moyale Precious Gems and Minerals Enterprises.

Wakili Hilla: Ni lini ulimpigia simu na kumhoji?

Shahidi: Nilimpigia Desemba 2, mwaka 2011, lakini alisema atakuja kesho yake na wakili wake aitwaye Tilatwa ambapo waliniambia watakuja saa sita.

Wakili Hilla: Ulimhoji kwa kosa gani?

Shahidi: Nilimhoji kwa kosa la kusaidia kutakatisha fedha haramu ila ilipofika saa nane mchana, aliomba tuahirishe kwani alikuwa anataka kwenda hospitali kutibiwa na hapo nikampa dhamana.

Wakili Hilla: Nini kiliendelea.

Shahidi: Aliendelea na dhamana yake hadi kesho yake alipofika kituoni saa tatu asubuhi na tuliendelea na mahojiano hadi saa 11 jioni.

Wakili Hilla: Mlifanya nini baada ya kukamilisha maelezo hayo?

Shahidi: Tuliendelea kumpa dhamana kwani tuliona ni mwaminifu na sasa naomba mahakama ipokee maelezo haya kama kielelezo cha ushahidi.

Katika hatua nyingine, shahidi huyo akiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyakomya, alidai baada ya uchambuzi wa awali, waliiandikia barua Serikali ya Marekani kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiomba Serikali hiyo kutoa ushahidi na vielelezo vitakavyosaidia katika kesi hiyo ambapo vielelezo hivyo vilianza kutumwa nchini Septemba mwaka 2012.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo itakapoendelea tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles