29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Jafo awataka maafisa Mazingira kusimamia kampeni ya soma na mti

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Seleman Jafo amewaagiza Maafisa Mazingira nchini kusimamia kampeni ya ‘soma na mti’ ambayo lengo lake ni wanafunzi wa shule za msingi Sekondari na Vyuo kupanda miti zaidi ya milioni 14 ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Pia amesema ukosefu wa mvua katika siku za hivi karibuni umesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kuna wajibu wa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko hayo.

Akizungumza leo Alhamisi Januari 20, 2022 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na vyuo nchini iitwayo soma na mti, Jafo amewaagiza Maafisa Mazingira hao kuisimamia kwa vitendo kampeni hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha miti mingi inapandwa nchini.

Waziri Jafo amesema ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) inazitaka kila Halmashauri kuhakikisha inapanda miti milioni 1.5 lengo likiwa ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchini hivyo kwa upande wa kampeni ya upandaji miti kupitia wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na vyuo wamepanga kupanda miti zaidi ya milioni 14.

Amesema lengo ni mwanafunzi ajivunie kwamba yeye amepanda pamoja na kuutunza mti kwa ajili ya utunzaji wa mazingira katika shule na vyuo.

Katika hatua nyingine,Waziri Jafo amesema ukosefu wa mvua katika siku za hivi karibuni umesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kuna wajibu wa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko hayo. 

“Mvua ilikuwa inaanza kunyesha kuanzia mwezi Septemba leo tuna Januari lakini mvua haijaanza hii ni kutokana na mabadiliko ya tabianchi kiwango cha maji katika mabonde na mito yetu yamepungua pia mgawo wa umeme umerudi kutokana na maji kupungua,”amesema Jafo.

Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anaeshughulikia elimu, David Silinde ameagiza kufufuliwa kwa Klabu za utunzaji wa mazingira katika shule pamoja na Maafisa elimu kuisimamia kwa vitendo kampeni ya soma na mti kuhakikisha inatekelezwa kikamilifu.

“Naziagiza shule zote nchini kuanzisha na kufufua Klabu za mazingira hili ni takwa na wala sio ombi nitahakikisha hili tunalitekeleza,”amesema Silinde.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Chilo amesema lengo la kuzindua kampeni hiyo ni kuhami viumbe hai, kutekeleza ilani ya CCM pamoja na kufuata matakwa ya sheria, hivyo amewaomba Watanzania kutunza mazingira na kwao liwe zoezi endelevu.

Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka aliwataka wale wenye viwanja vipya kupanda miti mitatu katika viwanja hivyo ikiwemo wa kivuli na mti mmoja na miwili ya matunda huku akidai kwamba agenda ya utunzaji wa mazingira katika mkoa huo ni endelevu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (CWT), Deus Seif amesema wapo pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan nakwamba kwa upande wa walimu kazi inaendelea.

Naye, mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka shule ya sekondari Dodoma, Monica Marwa ameiomba serikali kuchimba kisima katika shule ya Dodoma Sekondari ili wanafunzi waweze kumwagilia miti ambayo itapandwa huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawekea mazingita wezeshi ya kijifunzia na kusomea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles