Na Derick Milton, Simiyu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Suleiman Jafo ametoa muda wa wiki mbili kwa Mkandarasi Suma JKT kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa mradi wa viwanda viwili katika Halmashuari ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu.
Mradi huo unahusisha kiwanda kimoja cha chaki na kingine cha vifungashio, vyote vikiwa ni miradi ya halmashauri hiyo.
Jafo ametoa maagizo hayo leo Januari 3, baada ya kutembelea mradi huo, ambapo amekerwa baada ya kukuta hakuna kazi inayofanyika, huku baadhi ya vifaa vikiwemo vyuma vikiwa na kutu.
Jafo amesema kuwa mkandarasi huyo anafanya uzembe katika ukamilishaji wa mradi huo, ambapo amemtaka kuhakikisha ndani ya wiki mbili kuanzia leo anakamilisha ujenzi huo.
“Nimechukia sana baada ya kuona hali hii ya mkandarasi, baadhi ya vyuma vina mpaka kutu, hii inaonyesha hakuna kazi inayofanyika hapa, natoa wiki mbili kazi hii ikamilike,” amesema Jafo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashuari hiyo, Dk. Fredrick Segamiko amemweleza Waziri Jafo kuwa Mkandarasi huyo tayari ameongezewa muda mara tatu lakini ameshindwa kukamilisha.
“Januari 5, 2021 ndio ilipaswa kuwa siku ya mwisho ya nyongeza ya mara ya tatu ya muda ambao tulimpatia, lakini dalili hazionekani kama atamaliza, mradi huu unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 3.7 na tumemlipa, hatudai,” amesema Segamiko.
Aidha, akiwa katika Halmashuari ya mji wa Bariadi, Waziri Jafo ameupongeza uongozi wa halmashuari hiyo kwa ujenzi bora wa stendi ya mabasi wilayani humo ambayo amesema ni moja ya kati ya stendi nzuri na bora nchini.