28.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

Jafo asema agenda ya amani ni muhimu kwa Watanzania

Na RAMADHAN HASSAN

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo amesema wakati huu nchi ikijiandaa na uchaguzi mkuu, agenda ya amani ni muhimu kwa kila Mtanzania.

Pia amesema ili maonesho ya Nanenane yawe na tija,lazima halmashauri nchini zitumie maarifa ambayo yanapatikana katika maonesho hayo kuyapeleka kwenye jamii.

Kauli hiyo aliitoa juzi, wakati akifungua maonesho ya kilimo
na mifugo ya Nanenane Kanda ya Kati yanayoendelea kufanyika eneo la Nzuguni.

Maonyesho hayo yanajumuisha mikoa ya Singida na Dodoma.

Alisema wakati nchi ikijiandaa na uchaguzi mkuu, agenda ya amani ni muhimu kila Mtanzania anapaswa kuhakikisha anailinda na kuhakikisha uchaguzi unakuwa wenye amani.

“Wakati huu tukielekea uchaguzi, agenda ya amani ni muhimu sana lazima tuhakikishe kila mmoja anailinda amani ambayo tunayo,sio la kulifanyia mchezo,”alisema Jafo.

Alizitaka halmashauri zitumie maarifa ambayo yanapatikana katika maonesho hayo kuyapeleka katika jamii ili maonesho hayo yawe ni yenye tija kwa taifa.

Alisema kama maarifa na mafunzo yanayopatikana katika maonesho hayo yatapelekwa katika jamii kwa asilimia 75 anaamini nchi itapata mafanikio makubwa.

“Imani yangu kama mafunzo haya yatatumika hata kwa asilimia 75 tutapata mafanikio.Maarifa hayajatumika vizuri tuende katika utekelezaji kwa vitendo,nina amini tutafika mbali ndani ya miaka mitano, tutaingia katika uchumi wa kati ule endelevu tofauti na huu wa sasa,”alisema Jafo.

Aliwataka wafanyabiashara kufungua viwanda vingi vya minofu ya samaki katika ukanda wa Pwani tofauti na sasa ambapo viwanda vingi vipo kanda ya ziwa.

“Wenzetu wa utafiti na uwekezaji tuendelee kutafuta fursa katika viwanda vya minofu hasa katika ukanda wa Pwani kwenye nyama, tayari kuna viwanda vingi,tuende kwenye samaki sasa watu wafuge tufungue viwanda tuwawezeshe vijana wafanye kazi,”alisema.

Aliwaomba watafiti kuongeza utafiti wenye tija ambao utalisaidia Taifa kupata takwimu sahihi ambazo zitasaidia kupanga mipango endelevu na yenye faida kwa nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Rehema Nchimbi alisema mkoa wake si kama kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, wameanzisha kilimo cha korosho na parachichi ambacho kinastawi vizuri.

“Sisi ndio makao makuu mwenza na Dodoma,tupo vziuri,hakuna njaa tena kutokana na darasa hili la Nanenane,”alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge alimwomba Jafo maonesho yajayo yafanyike kitaifa mkoani kwake kutokana na kuwa makao makuu ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,637FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles