Jafo amsimamisha kazi mratibu Tarura Rukwa

0
949

Gurian Adolf -Sumbawanga

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, ameagiza kusimamishwa kazi kwa muda wa wiki mbili mratibu wa Tarura Mkoa wa Rukwa, Bonifas William, ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma dhidi yake ya kutoa zabuni ya matengenezo ya barabara mkoani humo kwa upendeleo jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.

Agizo hilo alilitoa jana wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuipa mwezi mmoja halmashauri hiyo kuwa imehamisha ofisi zake zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga na kuhamia katika mji mdogo wa Laela.

Alisema kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kuwa Tarura mkoa imekuwa inatoa zabuni za utengenezaji wa barabara mkoani humo, hivyo amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Joseph Nyamuhanga kumsimamisha kazi

Aidha Jafo pia ameziagiza halmashauri zote nchini ambazo madiwani walipitisha maazimio kuwa zihame katika maeneo zilizopo kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi, zifanye hivyo katika kipindi cha mwezi mmoja.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kutekeleza agizo hilo la Rais Magufuli pamoja na kuona wananchi hawapati usumbufu pindi wanapohitaji huduma kutoka katika halmashauri zao.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Mathias Nyange, alisema tayari Jeshi la Polisi linamshikilia Mkurugenzi wa Kampuni ya Fally Enterprises Ltd, Felix Lyowa ambaye juzi Rais Magufuli aliagiza akamatwe na kuchukuliwa hatua kutokana na kutekeleza mradi wa Laela wenye thamani ya Sh bilioni 1.7 chini ya kiwango.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here