27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Jafo aagiza ujenzi Soko la Sabasaba uanze kabla Juni

Ramadhan Hassan -Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ameagiza ujenzi wa Soko la Sabasaba jijini Dodoma uanze kabla ya Juni.

Agizo hilo alilitoa jana jijini hapa baada ya kutembelea soko hilo kujionea hali ya uchafu.

Katika ziara hiyo, Jafo alijionea mifereji ya maji ya mvua ikiwa imejaa uchafu jambo ambalo linahatarisha afya za wafanyabiashara wa eneo hilo.

Akizungumza na wafanyabiashara wa soko hilo, Jafo alisema hakutarajia kushuhudia soko la aina hiyo linalohatarisha afya za watu kwenye jiji linalokusanya mapato zaidi ya Sh bilioni 71.

“Nataka soko la Sabasaba kabla ya mwaka wa fedha kuisha ujenzi uanze, mrekebishe mazingira ya wafanyabiashara, haiwezekani mkusanye zaidi ya Sh bilioni 71 halafu mkaliacha hili soko hivi,” alisema Jafo.

Aliutaka uongozi wa jiji hilo kuachana na ujenzi wa hoteli ya nyota tatu unaofanyika ili wakaboresha mazingira ya wafanyabiashara wa soko hilo.

Jafo aliutaka uongozi huo kuhakikisha wanasimamia usafi na kuhakikisha mitaro inasafishwa ili kulinda afya na usalama wa  wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mkufya Msekeni, alisema tayari jiji limeshaandaa mchoro kujenga soko hilo.

Awali mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Za Asubuhi, alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakizungumzia suala la uchafu katika soko hilo, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Hili soko wafanyabiashara wa Majengo na Chang’ombe wanakuja kuchukua bidhaa, lakini limetelekezwa halifanyiwi usafi, mifereji ya kupitishia maji hakuna, mazingira kwa ujumla ni chafu kipindupindu hapa kipo nje nje, waziri tunaomba utusaidie,” alisema Za Asubuhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles