Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WAZIRI wa Katiba na Sheria, George Simbachawene amewashauri Watanzania kupeleka malalamiko yao katika Tume ya Haki za Binadamu badala ya kukimbilia Polisi huku akiwataka viongozi mbalimbali kuwaelekeza jambo hilo.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumatatu Februari 7, jijini Dodoma katika kikao chake na uongozi na watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu ambapo Waziri huyo amesema angetegemea chombo hicho kingekuwa maarufu lakini anashangaa wengi hawajui kama kuna sehemu ya kupeleka malalamiko yao.
Amesema wengi wamekuwa na utaratibu wa kupeleka malalamiko polisi wakati Tume ya Haki ya Haki za Binadamu ipo, hivyo anaamini ni wakati sasa wa kupaza sauti watu wengi waweze kwenda katika Tume hiyo.
“Bahati mbaya hampati wateja ningetegemea kuona chombo hichi kinakuwa maarufu kwani kina uwezo wa kuchunguza na kushtaki,”amesema Simbachawene.
Aidha,Waziri huyo amesema Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tume hiyo ikiwemo kuhakikisha taarifa za mwaka za Tume zinawasilishwa bungeni.
“Niwahakikishie Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kufanya kazi na Tume ya Haki za Binadamu na tutahakikisha taarifa zote zinawasilishwa bungeni kwani haki za binadamu ndio haki za mwenyezimungu,”amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amesema wanajiandaa kufanya uchunguzi wa matukio mabaya ya mauaji huku akidai wanakabiliwa na changamoto za ufinyu wa bajeti, uchache na uchakavu wa magari na taarifa za mwaka za Tume kutowasilishwa bungeni.