Basi lililokuwa limebeba watoto wa shule 51 lilitekwa na dereva wake na kisha kuchomwa moto karibu na Milan nchini Italia.
Watoto hao wa shule, baadhi yao walifungwa kamba, waliokolewa baada ya kuvunjwa vioo vya basi hilo upande wa nyuma na hakuna hata mmoja aliyejeruhiwa vibaya. Watu kumi na wanne waliathiriwa na moshi uliotokana na kuteketea kwa basi hilo.
Inaarifiwa kuwa dereva wa basi hilo mwenye miaka 47 na mwenye uraia wa nchini Italia ingawa ana asili ya kutoka nchini Senegal, ametiwa nguvuni.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaa Mkuu wa mjini Milan, Francesco Greco, awali kabla ya tukio dereva huyo alisikika akitamba, akiwaambia waliokuwemo katika basi hilo kwamba hakuna hata mtu mmoja atakaye nusurika.
Makundi mawili ya wanafunzi waliokuwa wakisindikizwa na waalimu wao , walikuwa wametoka mazingira ya shule iitwayo Vailati di Crema wakielekea mazoezini lakini baadaye gari ikachukua muelekeo tofauti na safari yao na kuelekezwa kwenye barabara kuu kufuata njia inayoelekea katika uwanja wa ndege wa Milan Linate, ripoti za mashuhuda zinaarifu .
Taarifa kutoka nchini Italia zinaarifu kuwa mafuta ya petroli yalinyunyizwa kulizunguuka basi hilo la shule , lakini polisi walitumia mbinu ya kuvunja madirisha ya nyuma ya basi hilo na hivyo kuwaruhusu abiria kushuka kwa haraka kabla basi hilo halijalipuka moto.
Waendesha mashitaka wa Milan wameeleza kuwa wanafanya uchunguzi wa kina kuchunguza ikiwa kulikuwa na nia zozote mbaya ikiwa ni pamoja na ugaidi.Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Matteo Salvini, alizungumza kwa hasira kwamba dereva huyo alikuwa na rekodi ya uhalifu.