Na Hadia Khamis, Mtanzania Digital
Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeeleza umuhimu wa wakulima na jamii kupata elimu ya kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yameelezwa jana katika maonesho ya 29 ya Nane Nane yanayofanyika Mbeya na Mhadhiri ambaye pia ni Afisa Mratibu wa kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia, Rufina Khumbe.
Amesema kituo hicho kinatoa ushauri kwa wakulima kujiandaa na matokeo chanya au hasi kulingana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoweza kuleta majanga.
“Wanaweza kutokea wadudu au mvua zisizotosheleza, kwa hiyo sisi tunatoa elimu na ushauri wapi watapata msaada endapo matatizo kama hayo yatajitokeza na tunawaelekeza namna ya kukubaliana na kuendana na matukio kama hayo,” amesema Rufina.
Amesema wakati mwingine unakuta mtu alichukua mkopo lakini anashindwa kufanya marejesho kama inavyotakiwa hatua ambayo inaweza kumsababisha kuchukua maamuliz magumu iwapo hatapata msaada wa mtu wa kuzungumza naye.
Ameongeza kuwa ni jukumu lao kutoa elimu na ushauri ili jamii iweze kujikinga au kukabiliana na matatizo yanayoweza kujitokeza.
“Jamii iboreshe mawasiliano kwa maana ya kuzungumza na kuibua changamoto baina yao katika jamii husika na kuona namna ya kuzitatua,” amesema.
Ameongeza kuwa uhusiano ni muhimu sana katika ngazi ya familia, kama wanafamilia hawataweza kuzigeuza changamoto na rasilimali walizonazo kuwa fursa ni dhahiri kwamba migogoro itajitokeza katika familia husika.
“Shida kubwa ni familia kutokuwa na mawasiliano au kuzungumza. Mfano katika suala la uchumi ambapo wana ndoa wanaweza kukaa chini na kuzungumza na kuweka bayana kipato chao ambapo familia ingeweza kuona namna sahihi ya kutumia kipato kinachopatikana kwa ajili ya kujikimu kimaisha na kusonga mbele,” amesema Rufina.
Wakati huo huo, Itika Ngwaka, Mhadhiri Msaidizi ambaye anafundisha masuala ya ustawi wa jamii amesema wameshiriki katika maonesho hayo kwasababu Wizara ina mpango wa kuboresha maisha ya Watanzania hususan kwenye eneo la kilimo na ufugaji na kufikia ajenda ya kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
“Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na maafisa ustawi wa jamii katika maeneo ya shughuli za kilimo kuisaidia jamii kuwa na familia zenye utulivu, kuepuka migogoro na kuwa na utulivu wa afya ya akili ili kuwawezesha kujikita katika kilimo hai na kujiandaa kisaikolojia kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na majanga yanayoweza kujitokeza kama ukame, wadudu waharibifu, na mafuriko. Sambamba na hilo ni kuiwezesha jamii kutambua wadau wa kilimo na fursa zilizopo ili ijikite kwenye kilimo hai na kufikia malengo,”amesema Rufina.
Amesema kwa muktadha huo pia tunahitaji watoto wa wakulima kujiunga na masomo ya elimu ya juu ili wakirudi katika kaya zao waweze kuboresha na kuendeleza shughuli za kilimo.