MSANII pekee wa Bongo Movie, Irene Uwoya, ameibuka kidedea kwenye uteuzi wa wagombea ubunge wa viti maalumu uliokamilishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) jana.
Uwoya alipata nafasi hiyo baada ya jina la mtoto wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, ambaye pia ni mgombea wa CCM katika jimbo la Ubungo, Dk Didas Masaburi, Juliana Masaburi kukatwa.
Mtoto huyo wa Masaburi, alishinda kura za maoni kupitia kundi la Vijana akiwakilisha Mkoa wa Mara lakini baada ya kukatwa nafasi yake ikachukuliwa na Irene Uwoya.
Awali mwigizaji huyo aliibuka kidedea kwenye kura za maoni jimbo la Tabora mjini kwa kupata jumla ya kura 34 akafuatiwa na Mariam Khamis aliyepata kura tatu na Zahara Michuzi aliyeambulia kura mbili.
Uwoya anakuwa msanii pekee wa Bongo Movie aliyeshinda nafasi hiyo baada ya wasanii wenzake, Wema Sepetu, Keysher na Steven Mengele (Steve Nyerere) kuangushwa kwenye ngazi tofauti.