TEHRAN, IRAN
KIONGOZI mkuu wa kiroho Iran, Ayatollah Ali Khamenei ameishutumu Marekani kwa kujaribu kuutanua mzozo ulioko Mashariki ya Kati.
Alisema Marekani imekuwa ikiichochea Saudi Arabia ambayo ni hasimu wa Iran kuikabili nchi hiyo.
Khamenei amesema njia moja ya kuikabili Iran ni kuwachochea watawala wasio na ujuzi wa ukanda huo ili kuanzisha mizozo zaidi na kuwasukuma Waislamu kupigana wenyewe kwa wenyewe.
Iran imesema ushirikiano kati ya Saudi Arabia na Marekani utaiyumbisha zaidi Mashariki ya Kati na kusisitiza Iran itaendelea kustawi ukanda huo licha ya juhudi za Marekani kutaka kupunguza ushawishi wake.
Kauli yake inakuja huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo juzi alikaririwa akisema nchi yake inatiwa wasiwasi mkubwa na vitendo vya Iran vinavyosababisha misukosuko Mashariki ya Kati.