32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

India wanawahi kuzeeka kuliko Japan, Uswis

HASSAN DAUDI Na MITANDAO

UTAFITI mpya uliochapishwa katika jarida la afya la Lancet Public Health, umebaini kuwa raia wa India huanza kukumbwa na dalili za uzee wakiwa na umri mdogo kuliko raia wa nchi za Japan na Uswis.

Utafiti huo ambao taarifa zake zilikusanywa kuanzia mwaka 1990 hadi 2017, ukihusisha mataifa 195, umebaini kuwapo kwa pengo la umri wa miaka 30 kati ya wananchi wa India na mataifa hayo mawili.

Lengo la utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Washington nchini Marekani kupitia taasisi yake ya Health Metrics and Evaluation (IHME), ni kubaini matatizo ya kiafya yanayowasumbua wananchi wa kila nchi kulingana na umri wao.

Ndipo watafiti walibaini kuwa mtu mwenye umri wa miaka 46 kule India, hatofautiani na wa miaka 76 nchini Japan linapokuja suala la kusumbuliwa na magonjwa ya ‘uzee’.

Magonjwa hayo ni pamoja na kutoona vizuri, shinikizo la damu, kupungua kwa uwezo wa kufikiri, moyo, kuvuja damu katika ubongo au hata viungo kama miguu kushindwa kufanya kazi ipasavyo.

Mbaya zaidi, kwa India ni kwamba wananchi wake huanza kukabiliwa na hali hiyo hata kabla ya kufikisha umri wa miaka 60.

“Matatizo ya afya yatokanayo na umri husababisha watu kustaafu, kupungua kwa nguvu kazi na matumizi makubwa ya fedha katika kushughulikia matibabu,” anasema Angela Y Chang, aliyekuwa kiongozi wa utafiti huo.

Hilo la India lina uhusiano mkubwa na hali ya kiuchumi nchini humo, ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa watu zaidi ya milioni 269 wanaishi katika lindi la umasikini.

Mfano mzuri ni changamoto ya uhaba wa maji inayolikabili taifa hilo kwa sasa, tafiti zikianika kuwa hali itakuwa mbaya zaidi kufikia mwaka 2020 kwani miji 21 haitakuwa na vyanzo vya rasilimali hiyo.

Kwa mantiki hiyo basi, utafiti huo umependekeza kuwa ni wakati wa viongozi wa serikali na wadau wengine wa afya nchini India kuona namna watakavyoweza kulivaa na ikiwezekana kupunguza ukubwa wa tatizo lililopo.

“Ni utafiti mzuri. Lazima mamlaka ziufanyie kazi. Hilo la kupungua kwa umri wa maisha ni tishio kwa jamii,” anasema Chang.

Ukiacha Japan na Uswis, nchi zingine ambazo bado zina wastani mkubwa wa umri wa kuishi kwa wananchi wake ni Ufaransa, Singapore, Kuwait, Korea Kusini, Hispania, Italia, Puerto Rico na Peru.

Wakati huo huo, Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Lesotho na Guinea-Bissau zimeingia katika orodha ya nchi ambazo wananchi wake wana wastani mdogo wa umri wa kuishi.

“Pia, hilo ni tatizo kwa nchi ikiwa wananchi wake wanakumbana na magonjwa ya umri mkubwa wakiwa chini ya miaka 60. Ni mzigo kwa serikali linapokuja suala la huduma za afya,” anaongeza msomi huyo.

Itakumbukwa kuwa utafiti wa mwaka juzi ulionesha kuwa wananchi wa Papua New Guinea walikuwa na wastani mzuri wa umri wa kuishi kuliko Uswis, wakati Algeria iliweza kuizidi kete Marekani.

Ni katika utafiti huo ndipo ilipoonekana kuwa kipindi hicho, kwa maana ya mwaka 2017, nchi 108 duniani kote zilikuwa na tatizo la wananchi wake kupata matizo ya afya yatokanayo na umri mkubwa.

Hata hivyo, ilionekana kuwa India ikiongozwa na China zimekuwa zikifanya vizuri katika kushughulikia maradhi yatokanayo na umri mkubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles