29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 18, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Imani potofu zafifisha mapambano dhidi ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele

Na Esther Mnyika, Mtanzani Digital

Wizara ya Afya imeeleza kuwa imani potofu zinazokuwepo katika jamii zinaathiri juhudi za kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, kama matende, mabusha, na trakoma, licha ya hatua kubwa zilizofikiwa.

Akizungumza Januari 21, 2025, jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP), Dk. Faraja Lyamuya, alisema serikali imefanikiwa kupunguza maambukizi ya magonjwa hayo chini ya asilimia mbili katika halmashauri 114, ikiwemo Kinondoni, Mtama, Pangani, Lindi, na Mikindani.

“Imani potofu kwamba magonjwa haya ni ya urithi, yametokana na kulogwa, au yanaathiri ukanda wa Pwani pekee si za kweli. Magonjwa haya yanatibika, na yeyote katika maeneo yenye mbu wenye vimelea anaweza kuathirika,” alisema Dk. Lyamuya.

Kwa ugonjwa wa trakoma (vikope), Dk. Lilian Ryatura alisema halmashauri zenye maambukizi makubwa zimepungua kutoka 69 hadi 9 baada ya kuanzisha kingatiba ya Zithromax. Alisisitiza pia kuwa kope za bandia zinachangia matatizo ya trakoma kwa kusugua macho na kusababisha kovu.

Aidha, Dk. Mohamed Nyati alihimiza matumizi ya kingatiba za kichocho zinazotolewa shuleni na kwenye jamii, akisema ni njia bora ya kujikinga na ugonjwa huo.

Mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani, yanayoadhimishwa Januari 30, 2025, yaliangazia mbinu za kuelimisha umma na kuongeza uelewa wa kinga na tiba. Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Tuungane. Tuchukue hatua. Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
594,000SubscribersSubscribe

Latest Articles