Ilala kujenga barabara za lami

Charles-KuyekoNa Harrieth Mandari, Dar es Salaam

HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala imejipanga kujenga barabara zote kwa kiwango cha lami katika   mwaka 2016/17 na  ujenzi huo unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.

Hayo yalielezwa  Dar es Salaam jana na Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko  katika kikao cha Baraza la Madiwani la manispaa hiyo.

Alisema zimetengwa  Sh bilioni 93 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo.

“Fedha hizo tayari tumeshakubaliana na Benki ya Dunia ambayo imekubali kutupatia kama mkopo na zitatumika kujenga barabara na mifereji yote ambayo imekuwa ni mibovu kwa kipindi kirefu na kero kubwa kwa wananchi,”alisema Kuyeko.

Alisema katika mradi huo, manispaa inatakiwa kuchangia Sh bilioni nane kama mkopo kutoka benki ambazo zipo tayari ingawa kinasubiriwa kibali kutoka TAMISEMI  kama sheria inavyotaka.

“Fedha zitakazotolewa na Benki ya Dunia ambazo ni Sh bilioni  93 zitasaidia ujenzi huo na    manispaa itachangia Sh bilioni nane  kwa ajili ya fidia kwa wananchi waliojenga pembeni mwa barabara hizo,”alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Greyson Celestine,  alisema tangu sera ya elimu bure ianze kutekelezwa, Manispaa  ya Ilala imepunguza tatizo la madarasa  ambako   vyumba vya madarasa 126 vimekwisha kujengwa katika shule 27.

“Kwa upande wa madarasa tumeshajenga madarsa 126,  malengo ya manispaa yakiwa ni kujenga madarasa  500,” alisema.

Manispaa hiyo ililenga kukusanya mapato ya   Sh bilioni 13.64 kwa   mwaka 2016/17 na  katika kipindi cha robo ya mwaka tayari imeshavuka lengo na kukusanya Sh bilioni 16.09.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here