WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, amewasilisha makadirio ya bajeti ya Sh bilioni 585 kwa ajili ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 20 zimetengwa kwa ajili ya Ofisi ya Rais (Ikulu), ikiwa ni matumizi ya kawaida kwa ajili ya ofisi hiyo na taasisi zake.
Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jana, Kombani alisema katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 Ikulu imepanga kutekeleza kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa huduma kwa rais na familia yake.
Kazi nyingine ni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano Ikulu na kuanza maandalizi ya ujenzi wa jengo la mapokezi upande wa baharini. Nyingine ni ukarabati wa Ikulu ndogo mkoani Mbeya na maandalizi ya ujenzi wa Ikulu ndogo, Zanzibar.
“Kutoa huduma za ushauri kwa rais katika maeneo ya uchumi, siasa, masuala ya jamii, sheria, mawasiliano, uhusiano wa kimataifa, mawasiliano na habari kwa umma. “Kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership).
“Kuendelea kuratibu na kusimamia miradi ya maendeleo ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea,” alisema.
Kuhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kombani alisema katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 taasisi hiyo inakusudia kutekeleza kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuchunguza tuhuma 2,776 zilizopo.
Kazi nyingine ni kukamilisha uchunguzi wa tuhuma 10 za rushwa kubwa (Grand Corruption) kama ilivyopangwa katika mpango mkakati wa taasisi hiyo.
“Kufuatilia na kudhibiti vitendo vya rushwa katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi. “Kuandaa mafunzo maalumu kwa waheshimiwa majaji na mahakimu kuhusu Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura 329 na Sheria namba 6 ya mwaka 2010 ya Gharama za Uchaguzi na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.