24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

IJEBA: Kikundi chenye ndoto ya kulisha Dodoma

0d6a5588NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

JULAI, 23 mwaka huu Rais Dk. John Magufuli, alitangaza azimio la Serikali yake kuhamia Dodoma.

Rais Magufuli alitoa tamko hilo katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao agenda yake kuu ilikuwa ni kupokea kijiti cha uenyekiti wa chama hicho kutoka Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Serikali kuhamia Dodoma ni fursa kwa wananchi wa mkoa huo hasa wajasiriamali ambao watanufaika na fursa mbalimbali zitakazojitokeza.

Kwa kuliona hilo mapema, kikundi cha Ibua Jenga Badilika (IJEBA) kilichopo Kata ya Soya, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kimeanzisha miradi mbalimbali ambayo itasaidia kuwakwamua vijana kutoka katika lindi la umasikini.

Kikundi hicho kinachojishughulisha na miradi ya kilimo na ufugaji, kimesajiliwa Machi 2016 wilayani Chemba na kupata namba yake ya usajili CDC/CD/2016/CBO- 316, ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti ya kikundi katika Benki ya CRDB.

Mwenyekiti wa IJEBA, Shaaban Isere, anasema kikundi hicho kilianza mwaka 2015 kikiwa na wanachama 10, lakini sasa kina wanachama 15 ikiwa ni ongezeko la asilimia 50.

Anasema kikundi hicho kinajihusisha na masuala ya kilimo na ufugaji ikiwa ni pamoja na kumiliki duka moja la pembejeo za kilimo.

“Kwanza tunamshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa agizo la Serikali yake kuhamia Dodoma, hii ni neema na fursa kwa wananchi wa Dodoma na wilaya zake, sasa tunauhakika wa soko,” anasema.

Akizungumzia historia ya kikundi hicho, Isere anasema. “Wakati tunaanza tulikuwa na kuku 10 tu, lakini hivi sasa wamefikia 70 ikiwa ni ongezeko la asilimia 700. Mbuzi walikuwa wanne na sasa wamefika 14 na kuwa asilimia 350.

“Malengo yetu ni kuhakikisha kikundi kiweze kukua, ili tuweze kuchangamkia fursa ya ujio wa Serikali katika mkoa wetu wa Dodoma, kwani hivi sasa uzalishaji ni mdogo,” anasema.

Isere anasema kikundi hicho kinamiliki shamba la ekari sita, ambapo wanafanya kilimo cha mboga mboga kama vile mchicha, matembele, kabichi, majani ya maboga, bamia, nyanya chungu, bilinganya, vitunguu na nyanya.

Anasema pamoja na kufanya miradi hiyo pia wamekuwa wakijihusisha na utoaji wa elimu ya ukimwi kutokana na kuwa kikundi chao kina mchanganyiko wa wazee na vijana ambao ndio nguvu kazi wanayoitegemea.

Anasema lengo la kuanzisha kikundi hicho ni kutekeleza agizo la Serikali la kutaka wananchi kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kuweza kusaidiwa na kujengewa uwezo katika ujasiriamali.

Changamoto

Isere anasema pamoja na jitihada wanazofanya kuhakikisha kikundi kinafikia malengo yake, lakini wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali ambazo zinarudisha nyuma jitihada za kikundi.

Anazitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa mtaji wa kuwawezesha kukuza miradi yao waliyoianzisha kwa nguvu zao wenyewe.

“Sisi tunatamani kumiliki vifaa vyetu lakini uwezo wetu ni mdogo kwani hata duka letu la pembejeo thamani ya bidhaa zilizopo ni Sh milioni moja tu.

“Katika shamba letu, tunategemea zaidi mvua na mito ambayo wakati wa kiangazi hukuaka na hivyo kufanya tushindwe kufikia malengo ya uzalishaji wa mboga mbonga.

“Tunahitaji kulima kisasa, lakini tunashindwa kutokana na kukosa mtaji. Mkoa wetu wa Dodoma unajulikana ni mkoa wenye ukame, ili tufanye kilimo cha umwagiliaji tunahitaji kuwa na kisima chetu.

“Hapo inahitajika zaidi ya Sh milioni 30 kufanikisha kisima, fedha hizo kama kikundi hatuna. Napenda kutumia fursa hii kuziomba taasisi za Serikali au wadau wa maendeleo wasaidie juhudi za kikundi hiki ili vijana hawa waweze kujikwamua kimaendeleo, lakini pia kutimiza ndoto zao.

“Tumekwenda halmashauri kuomba watushike mkono kupitia fedha za makundi ya vijana, ambazo hutengwa kwa kazi hii ya kuwezesha vikundi kama hivi lakini hatujapata msaada wowote,” anasema.

Akizungumzia changamoto ya mbolea, Isere anasema. “Tumekuwa tukigombea mbolea na wateja katika duka la pembejeo, hivyo wakati mwingine tunajikuta tunakosa mbolea ya kuweka katika shamba la kikundi.

“Changamoto nyingine ni uhaba wa wataalamu wa masuala ya ufugaji na kilimo, kwani matarajio yetu sisi ni kufuga kisasa na kulima kilimo cha kisasa, lakini wataalamu hakuna,” anasema.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, vijiji vipo vinne katika maeneo hayo vyenye wakazi zaidi ya 20, 000 lakini mtaalamu anayetoa huduma za ugani ikiwamo kilimo na ufugaji ni mmoja tu.

Naye Katibu wa Kikundi cha IJEBA, Jeremiah Nyarasha, anazungumzia changamoto ya ubovu wa barabara ambazo zimekuwa kikwazo cha kusafirisha bidhaa zao pamoja na madalali.

“Madalali wamekuwa wakitukandamiza katika bei za uuzaji wa wanyama kwani tumekuwa tukitumia pesa nyingi katika kuihudumia mifugo yetu lakini bei tunazokuja kuuza ni ndogo na wanaofaidi ni madalali kwani wao huenda kuuza bei ya juu zaidi.

“Pia tunayo changamoto ya wizi wa mifugo, ukosefu wa maeneo ya malisho pamoja na mabanda ya kisasa ya kufugia.

“Ili kufanikisha malengo ya kikundi cha IJEBA tunaomba wadau mbalimbali wa maendeleo watusaidie ili tuweze kupiga hatua kutoka hapa tulipo,” anasema.

Jeremiah alitoa wito kwa vijana kuwa na mawazo ya kujiajiri wenyewe kwa kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, badala ya kukaa vijiweni na kutoa lawama kwa Serikali kwamba hakuna ajira.

“Fursa zipo nyingi ila vijana wengi bado wamelala wanasubiri ajira serikalini, jambo ambalo ni gumu kwani vijana wenye mahitaji ya ajira ni wengi na nafasi za kazi katika mashirika au kampuni binafsi ni chache.

“Hata hivyo kwa wale vijana waliojitambua na kuanzisha vikundi vyenye miradi kama hiki cha kwetu bado wanakabiliwa na tatizo la mitaji katika kukuza shughuli za ujasiriamali.

“Ndiyo maana tunaomba wadau wa maendeleo wasaidie kikundi chetu ili kiweze kutoa ushawishi kwa vikundi vingine vya Wilaya ya Chemba au wilaya jirani,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,476FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles