30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

IGP WA ZAMANI UGANDA APANDISHWA KIZIMBANI

KAMPALA, UGANDA


ALIYEKUWA Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Uganda, Kale Kayihura, amefikishwa katika mahakama ya jeshi ya Makindye jana kwa mashtaka kushindwa kulinda zana za kivita kati ya mwaka 2010 na 2018.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, IGP Kayihura, alitoa idhini silaha zitolewe kwa watu wasiostahili, kusaidia na kuhamishwa kiharamu kwa raia wa Rwanda waliopo uhamishoni.

Hata hivyo, Kayihura amekana mashtaka yote. Mawakili wake wameomba aachiliwe kwa dhamana na wametakiwa kuwasilisha ombi hilo kwa maandishi.

Kayihura alikamatwa Juni mwaka huu nyumbani mwake katika Kijiji cha Katebe wilayani Lyantonde na amekuwa kizuizini kwa miezi miwili sasa.

Jenerali Kale Kayihura, ambaye kwa wakati mmoja alikuwa mojawapo ya watu wenye nguvu nchini humo, ameishi katika kambi ya kijeshi huko Makindye iliyopo jijini Kampala.

Baada ya kuwasili ndani ya gari la Jeshi la Polisi, Kayihura, aliongozwa hadi ndani ya mahakama hiyo iliyokuwa imejaa watu pomoni.

Kayihura alionekana akitabasamu kiasi huku akiwa amevalia magwanda ya jeshi la taifa la Uganda People’s Defence Forces (UPDF).

Usalama uliimarishwa katika maeneo ya mahakama hiyo tofauti na siku za kawaida huku watu wote waliokuwa wakiwasili wakikaguliwa kwa kina mlangoni.

Nje ya mahakama hiyo kulikuwa na kundi la wafuasi wa kiongozi huyo wa zamani wakiwa wamevaa fulana zenye picha na ujumbe wa kuonyesha kumuunga mkono Kayihura.

Jenerali Kayihura alikuwa mkuu wa Jeshi la Polisi kwa takribani kwa miaka 12 kabla ya kutimuliwa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni.

Katika muda wake wa uongozi kama mkuu wa Jeshi la Polisi, idadi ya maofisa wa polisi iliongezeka zaidi ya maradufu.

Jenerali Kayihura, ambaye ni mkereketwa wa vita iliyomsaidia Rais Museveni kuingia madarakani mwaka 1986, kwa wakati mmoja alikisiwa kuwa ofisa mwenye mamlaka makubwa zaidi katika Jeshi la Uganda.

Makundi ya kutetea haki za binadamu nchini Uganda yalionekana kufurahia hatua ya kutimuliwa kwa Kayihura, wakisema Jeshi la Polisi lilikuwa limeshindwa kulinda usalama wa raia na mali zao chini ya uongozi wake.

Kesi ya Jenerali Kayihura inatarajiwa kusikilizwa tena mahakamani Septemba 4, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles