NENO Jeshi kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili sanifu toleo la tatu la mwaka 2013, ni askari wanaoajiriwa kulinda nchi na tafsiri ya pili ni wingi wa watu.
Ajabu katika maisha ya kawaida ya watu walio wengi wakiwamo Watanzania, wakisikia neno Jeshi tafsiri inayowajia haraka akilini mwao, ni chombo kinachotumia mabavu katika kulinda nchi.
Kama si sababu za kibaiolojia, basi kisaikolojia inawezekana tafsiri ya utumiaji mabavu katika Jeshi ni matokeo ya mfumo uliowakuza Watanzania kabla, wakati na baada ya Uhuru kwamba askari ni kifaa cha kuogopwa.
Mei 28, mwaka huu Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli alimteua aliyekuwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP)
Hakika uteuzi huu ulioendana na kumtengua aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi hapo awali, Ernest Mangu ambaye muda wake ulikuwa haujaisha, uliibua maswali mengi kuliko majibu.
Hata hivyo kitendawili cha utenguzi kimeteguliwa Juni 2, mwaka huu baada ya Rais kukutana na makamanda wote wa Polisi kutoka Tanzania Bara na visiwani jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo Rais amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Sirro kujipanga vizuri yeye na safu yake ya makamanda, viongozi wakuu wa vikosi na maofisa mbalimbali ili kuondoa dosari zote za utendaji kazi zinazoshusha ufanisi na heshima ya Jeshi la Polisi.
“Ni lazima ufanye mabadiliko makubwa, nataka kuona Jeshi la Polisi linakuwa Jeshi la Polisi, wewe IGP Sirro na makamnda wenzako hakikisheni mnakomesha uhalifu, komesheni mauaji dhidi ya raia, ujambazi na dawa za kulevya,” Rais alisisitiza.
Mbali na hilo, pia Rais amewataka makamanda, maofisa na askari wa Jeshi hilo kujiepusha na rushwa, dawa za kulevya, kutumiwa na watu kwa maslahi binafsi, kuingia mikataba isiyo na masilahi kwa Jeshi na Taifa, ubadhirifu na kuacha upendeleo katika utoaji wa ajira na vyeo.
Ni dhahiri haya yaliyotamkwa Rais hata kama kuna sababu nyingine lakini ndicho kiini cha kumteua Simon Sirro kuwa IGP. Hata hivyo ili Jeshi la Polisi liweze kukabiliana na vitendo vya uhalifu mkubwa, kitengo chake cha Upelelezi hakina budi kufanyiwa marekebisho makubwa.
Ni wazi kitengo hiki pamoja na mazuri yake, bado kinapwaya katika utendaji wake unaoweza kuwa unasababishwa na mfumo wa mafunzo kama si udhaifu binafsi wa kibinadamu.
Ni aibu, fedheha na usaliti kwa afisa upelelezi kujinadi ovyo ovyo mbele ya raia ili ajulikane yeye ni nani wakati angejichanganya kimya kimya angeweza kupata taarifa mbalimbali zikiwamo za uhalifu.
Ukiwa mitaani utaona watu wakiwanyoshea vidole wapelelezi kuwa huyo ni CID, mara afisa upelelezi. Kujulikana kwa namna hii kama si kukaa muda mrefu kituo kimoja basi ni huku kujitweza ili kupata misifa.
Naamini umaarufu hutafutwa na mwanasiasa ili kuwapata wafuasi wengi watakaompa ulaji, lakini umaarufu hauwezi kumsaidia mpelelezi kuwabaini wahalifu.
Wakati umefika IGP Sirro kuunda kikosi cha Upelelezi chenye mafunzo na uadilifu mkubwa kama wa FBI au CIA, kwani ubora wa Jeshi si wingi wa silaha au nguvu ya misuli ya askari kama raia baadhi wanavyoamini, bali ni mbinu na mikakati chanya inayoweza kutambua uhalifu na kuuzuia kabla haujaleta madhara katika jamii ikiwamo kuuawa askari kwa kushtukiza.