32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

IGP SIRRO SHUGHULIKIA CHANGAMOTO HIZI

AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Dk. John Magufuli, jana amemwapisha Mkuu wa Jeshi la Polisi mpya, IGP Simon Sirro.


Sirro anakuwa IGP wa 10 tangu taifa hili lipate uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1961. 
Anachukua nafasi ya Ernest Mangu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Magufuli juzi.


Mangu ametumikia nafasi hiyo tangu Desemba 30, 2013 baada ya kuteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. 
Katika utendaji wake, kila mmoja amejionea namna ambavyo amefanya kile alichokiweza.


Uteuzi wa IGP Sirro haukutegemewa na wengi, kwa sababu kwanza imekuwa ghafla, jambo ambalo limeonekana kushtua wengi na kujiuliza maswali mengi bila majibu.


Sisi wa MTANZANIA tunasema karibu IGP Sirro katika wadhifa huu mpya, ambao tunaamini utautendea haki kwa manufaa ya Watanzania wote.


Tunatambua utendaji kazi wako, tangu ukiwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga na Mwanza.
Tunatambua kazi kubwa uliyoifanya katika mikoa hiyo hadi uhalifu ukapungua kwa kiasi kikubwa.


Tunaelewa vizuri kipindi chote ulichokaa Mwanza, ulifanya kazi nzuri na kulifanya jiji hilo kuwa shwari tofauti na ilivyokuwa wakati wa mtangulizi wako aliyekuwapo hapo awali.


Lakini hata baada ya kupelekwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam katika kitengo cha intelijensia, bado ulifanya kazi vizuri hadi ukapandishwa cheo na kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ukichukua mikoba ya Suleiman Kova.
Umeonyesha namna ambavyo umepambana na matukio ya kanda yako, licha ya matukio ya uhalifu kuwapo karibu kila siku. 


IGP Sirro umepitia hatua nyingi hadi kufikia hapo, ikiwamo vita ya maneno kutoka kwa wanasiasa, lakini hatukusikia ukijibizana nao.
Tabia hii, inawezekana wazi ndiyo iliyomsukuma Rais Magufuli na jopo lake kukuteua kushika wadhifa huo mkubwa katika Jeshi la Polisi.


Pamoja na sifa zote hizo, IGP Sirro tunakukumbusha kuwa kuna changamoto kubwa mbele yako, ambazo inabidi ukabiliane nazo ili kuzipatia ufumbuzi.


Mosi, tumia uwezo wako kupambana na mauaji holela ya viongozi wa kisiasa, askari polisi na wananchi wa kawaida katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani.


Pili, tunakukumbusha ushughulikie mwenendo wa askari wako ambao katika siku za karibuni wamekuwa na tabia ya kupiga wananchi risasi na kuwapotezea uhai kwa visingizio kuwa ni majambazi. 


Vitendo hivi ambavyo katika siku za karibuni vimetokea maeneo ya Kurasini na Kigamboni mkoani Dar es Salaam, vinalichafua Jeshi la Polisi na kuondoa dhana ya kuwa jeshi hilo na wananchi si maadui.


Tatu, tunakukumbusha uchukuwe hatua dhidi ya utovu wa nidhamu unaofanywa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani ambao wamekuwa mabingwa wa kubambikizia watu makosa.


Sisi MTANZANIA, tunatambua uwezo wako mkubwa wa kiutendaji, tuna imani kubwa kwamba utaongoza jeshi hilo kwa uadilifu na umakini mkubwa ili kufikia malengo.


Tunamalizia kwa kusema uteuzi wako haukuja kwa bahati mbaya, onyesha kweli unaweza.
Tunataka kuona Tanzania bila mauaji na kurejesha nidhamu ya askari polisi inayoonekana kuporomoka.
Ni matumaini yetu kuwa utafanya kazi yako kwa weledi kuhakikisha Watanzania wanabaki salama pamoja na mali zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles