25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

IGP SIRRO BADO ANATAKIWA KUJIPANGA VYEMA

LEO umetimia mwezi mmoja tangu Mbunge wa Singida Mashariki  (Chadema), Tundu Lissu, apigwe risasi na watu ambao hadi sasa Jeshi la Polisi limeshindwa kuwabaini.

Tangu atoweke katika mazingira ya kutatanisha mwanasiasa wa Chadema, Ben Saanane, leo ni siku ya 330, Jeshi la Polisi linaonekana bado halina taarifa zozote za mahali alipo.

Leo hii ni miaka minne tangu ‘Watu Wasiojulikana’ wamtie kilema  Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd., Absalom Kibanda na miaka takribani 10 tangu mwanahabari Saed Kubenea amwagiwe tindikali.

Wakati tukio la Lissu likitimiza mwezi mmoja sasa, Jeshi la Polisi halijawatia hatiani waliopanga na kutekeleza shambulio lile lenye sura ya mauaji.

Hakuna yeyote aliyekamatwa kwa kuhusika na shambulio la Kibanda, wala matukio ya miili ya watu iliyokutwa imefungwa kwenye viroba na kisha kutupwa katika Mto Ruvu na hivi juzi juzi tu Bahari ya Hindi.

Mara tu baada ya kuapa kushika wadhifa wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,  Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, alipokutana na makamanda wa mikoa yote, viongozi na wakuu wote wa jeshi hilo, Rais Dk. John Magufuli alitoa wito kwa jeshi hilo kurejesha hadhi yake.

Katika kikao hicho ambacho kilifunguliwa na Rais Dk. Magufuli, alimtaka IGP Sirro pamoja na safu yake ndani ya Jeshi hilo kujipanga vizuri kwa maana ya kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji.

Zaidi na ambalo sisi tuliona limetugusa, ni kauli ya Rais Magufuli aliyosema kwamba, anataka kuona Jeshi la Polisi linakuwa Jeshi la Polisi, akitoa wito wa Sirro na wenzake kuhakikisha wanarudisha hadhi na heshima ya chombo hicho kwa kukomesha uhalifu.

Kauli hii ya Rais Magufuli si ya kwanza kuitoa na ni wazi ndicho kinachoonekana kwa wengi tu, tukitamani kuona Jeshi la Polisi linafanya kazi yake sawasawa ya kulinda raia na mali zao na pengine kuliko ilivyo hivi sasa.

Ukitaka kujua kwamba pengine Rais Magufuli alikuwa hafurahishwi na mwenendo wa Jeshi hilo, itakumbukwa hata kabla ya kauli hiyo,  aliwahi kukaririwa miezi kadhaa iliyopita wakati akizindua mpango wa kuboresha usalama wa jamii kwa Jeshi la Polisi kwa Wilaya ya Kinondoni, akimkumbusha IGP aliyepita, Ernest Mangu, umuhimu wa Jeshi la Polisi kurejesha hadhi yake kwa kuzingatia misingi ya kuanzishwa kwake.

Tunayakumbuka vyema maneno yake kwa Mangu juu ya matamanio yake siku moja kumpeleka mstari wa mbele endapo uhalifu utaendelea kukithiri pasipo hatua madhubuti kuchukuliwa.

Rais Magufuli alikuwa akielezea mshangao wake wa mambo kadha wa kadha yanayoendelea ndani ya Jeshi la Polisi, miongoni mwake ikiwa ni kitendo cha polisi kushindwa kutumia mbinu zao kunyang’anya silaha majambazi wanapofanya uhalifu.

Leo hii tunapokumbuka kauli hizo za Rais Magufuli na tunapoendelea kushuhudia matukio ya ajabu katika nchi yetu, tunadhani bado IGP Sirro anatakiwa kujipanga vyema ili kuleta sura halisi ya Jeshi la Polisi, ambayo wengi tunaitamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles