Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amewaonya watu waliopata msamaha wa Rais Dk. John Magufuli, katika sikukuu wa Muungano Aprili 26, mwaka huu kuchunga tabia na matendo yao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 24, wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo vya polisi vya kisasa vya Mburahati, Kiluvya, Gogoni na Mbweni IGP Sirro amesema nia ya rais kuwapa msamaha ilikuwa njema lakini kuna baadhi ya watu wameitumia vibaya fursa hiyo na hadi sasa watu watano wamekwishauawa na wananchi.
“Rais aliwapa msamaha baadhi ya watu lakini wametumia vibaya msamaha huo na kurejea kwenye matendo yao maovu ambapo hadi sasa watu watano wamekwishauawa na wananchi kutokana na matendo yao.
“Ukitoka gerezani kwa msamaha, maana yake umerekebisha mwenendo wako na wananchi wanatarajia uwe hivyo, lakini kama ukifanya vinginevyo, Serikali isilaumiwe,” amesema.