24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

IGP Sirro akiri kumsaka mume wa Zamaradi kwa kutishia kwa bastola

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, ameagiza kukamatwa kwa mtu anayedaiwa kuwa ni mume wa mtangazaji maarufu nchini, Zamaradi Mketema, ambaye ametajwa kwa jina la Shaban  kwa tuhuma za kumtishia dereva mwenzake silaha aina ya bastola.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Sirro alisema kuwa watu hupewa silaha kwa masharti maalumu na kwamba hawakuwapa ili wawatishie Watanzania.

IGP Sirro alisema tayari Jeshi la Polisi linamsaka kijana huyo licha ya kwamba amekuwa akiwakwepa kwepa.

Kauli ya IGP Sirro imekuja siku moja baada ya juzi jioni kusambaa video inayomwonesha Shaban aliyekuwa na gari dogo lenye rangi ya bluu akitishia kumpiga risasi dereva mwenzake aliyekuwa akiendesha gari kubwa.

IGP Sirro alisema kuwa licha ya kutofahamu sababu ya ugomvi uliosababisha kijana huyo kutoa silaha lakini suala la kujiuliza ni kama kulikuwa na ulazima kumtishia silaha.

“Tukibaini umetishia Watanzania kama alivyofanya yule kijana, hatujui ugomvi ulikuwa ni nini lakini je, kama ni kweli yale yaliyokuwa yanaelezwa kulikuwa na ulazima wa kutoa silaha kumtishia mwenzake?” Alihoji IGP Sirro .

“Kimsingi mtu ukipewa silaha hakikisha unafuata yale masharti, usipofuata masharti la kwanza tutakunyang’anya silaha, lakini la pili tutakupeleka mahakamani na la tatu tutamwomba Mungu tukufunge ili ukirudi nyumbani kwa mke wako au kwa mume wako uwe na adabu ya kutunza vitu vyako,” alisema IGP Sirro.

Katika video hiyo dereva wa gari kubwa alianza kusikika akimwambia dereva wa gari dogo (Shaban) kuwa; “umesema unatoa bunduki  itoe hiyo bunduki,”.

Wakati mzozo huo ukiendelea dereva wa gari dogo (Shaban) aliyekuwa amevaa shati jeupe alielekea kwenye gari lake na kutoka na bastola.

Licha ya dereva huyo kutoka na bastola yule wa gari kubwa ambaye alisikika akiongea kwa jazba hakuonesha kutishika na kitendo cha mwenzake kutoka na bastola na kumwambia kuwa kama anataka kumshambulia kwa bastola haogopi kwa sababu alizaliwa ni lazima atakufa.

“Mimi kufa nitakufa na wewe utakufa, huna lolote nakwambia kweli huna lolote, toa hiyo bunduki, mwache aniue,” alisikika akisema dereva wa gari kubwa.

Licha ya dereva wa gari dogo kumwamuru mwenzake akae chini huku akitukana matusi bado dereva huyo alikataa huku akisisitia kuwa kama anataka amuue.

Pia dereva huyo alionekana akimpiga mwenzake na bastola hiyo kichwani na kumweleza kuwa atampasua kwa kutumia silaha hiyo aliyokuwa ameishika.

Juhudi za gazeti hili kumtafuta Shaban ziligonga mwamba.

Zamaradi alipotafutwa kwa simu kuzungumzia kuhusu video hiyo na kama mtu anayeonekana humo ni mume wake, simu yake iliita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya mtandao wa Whatsapp licha ya ujumbe huo kusomwa haukujibiwa.

Mmoja wa watu wa karibu na mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Shaban ambaye hakutana jina lake liandikwe gazetini alithibitisha kuwa ni kweli kijana huyo ni mume wa Zamaradi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles