IGP Sirro ahimiza usajili kampuni za ulinzi mfumo PSGP

0
571

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro ameziagiza kampuni binafsi za ulinzi na wafanyakazi wa kampuni hizo kuhakikisha wamesajiliwa kwenye Mfumo wa  Kusimamia Sekta ya Ulinzi Binafsi (PSGP) hadi kufikia tarehe 31 Disemba 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki nchini jijini Dar es Salaam, baada ya kufanya kikao na wamiliki na wakurugenzi wa kampuni binafsi za ulinzi, alisema kuwa mfumo huo wa kusajili kampuni na wafanyakazi wake kwenye kanzi data maalum ndiyo njia ya kipekee ya kudhibiti changamoto katika sekta hiyo hususan askari wasio waaminifu.

IGP Sirro alisema kuwa mfumo huo ni mzuri na utaboresha sekta hiyo, lakini akasisitiza kuwa elimu zaidi inahitajika kwa wadau.

“Mfumo ni mzuri, lakini kitu kikubwa ni suala la elimu. Watu wakielimishwa nadhani wanaelewa, wakurugenzi wangu [wa makampuni binafsi ya ulinzi wana elimu kubwa na wamekwenda shule wakipata elimu ya kutosha wataukubali mfumo.

“Kwa sababu askari leo anafanya uhalifu kwenye kampuni hii na anakwenda kwenye kampuni nyingine kufanya kazi, sasa bila kuwa na mfumo huu huwezi kumtambua huyu askari kwamba ni mbabaishaji,” alisema IGP Sirro.

Aliwanyooshea kidole baadhi ya walinzi ambao huingia kwenye sekta hiyo wakiwa na lengo la kupeleleza njia zinazoweza kuwasaidia kufanya uhalifu na kwamba kupitia mfumo wa PSGP watadhibitiwa.

“Kuna baadhi ya askari hawa wa ulinzi binafsi anaingia kufanya kazi kwa lengo la wizi tu, anapelekwa kule anakuwa chambo kujua kinachofanyika ni kitu gani, lakini kwa kutumia mfumo [wa PSGP] ndiyo njia ya kipekee ya kuweza kudhibiti hili,” alifafanua.

IGP Sirro alisema kuwa amewaagiza wadau wa sekta hiyo ya ulinzi binafsi kukutana tena, kuhakikisha wanatatua dosari zilizopo ili wote kwa pamoja wakubaliane na mfumo huu.

Jeshi la polisi liliagiza kampuni zote binafsi za ulinzi pamoja na wafanyakazi wa kampuni hizo kuhakikisha wamesajiliwa kwenye PSGP kabla ya mwaka 2021 kwani baada ya Desemba 2020 wale ambao hawatakuwa wamesajiliwa kwenye mfumo huo hawataruhusiwa kufanya kazi kwenye sekta hiyo.

Zaidi ya kampuni 174 na wafanyakazi 14,000 wamesajiliwa kwenye mfumo huo hadi kufikia siku ya kikao hicho na usajili unaendelea katika mikoa yote nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here