Na Brighiter Masaki
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Simon Sirro amesema Jeshi la Polisi linaendeshwa kwa maandishi hivyo wanasubiri barua kutoka kwa Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima kuhusu maagizo ya kumkamata Askofu Josephat Gwajima.
Kauli hiyo ya IGP Sirro, amekuja baada ya waziri huyo kuliagiza Jeshi la Polisi na Takukuru kumkamata na kumhoji Mbunge wa Kawe, Askofu Gwajima.
IGP Sirro amesema maagizo hayo yameonekana mtandaoni hivyo wanasubiri agizo rasmi na kutekeleza agizo hilo na wataangalia kama kuna jinai kabla ya kufungua mashtaka mahakamani.
“Hatujapa taarifa rasmi ya maandishi ya kutakiwa kumkamata Gwajima, lakini hata tukiipokea tutachunguza iwapo matamshi yake yanaangukia kwenye jinai, lakini tunaweza kuwashauri wakatatua jambo hili kwa njia za mazungumzo badala ya Polisi.
“Sisi kama polisi hatuna nafasi ya kufanya lolote kumhoji mtu pale anaposema maneno yasiyo na jinai ndani yake,” amesema majibu ya IGP Simon Sirro
Dk. Gwajima ametoa agizo hilo kutokana na kauli za Askofu huyo a kupinga hadharani chanjo ya Uviko-19.