Kulwa Mzee -Dar es salaam
MSANII wa vichekesho, Idris Sultan na mwenzake wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakituhumiwa kushindwa kufanya usajili wa laini za simu.
Idris na Innocent Maiga wamesomewa mashtaka mawili jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.
Washtakiwa walisomewa mashtaka yanayowakabili na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, Matilda Mushi na Estazia Wilson.
Wankyo alidai mshtakiwa Idris katika kosa la kwanza anadaiwa kushindwa kufanya usajili wa simu kadi iliyokuwa inamilikiwa na mtu mwingine.
Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Desemba mosi, 2019 na Mei 19, 2020 maeneo ya Mbezi Beach Kinondoni ambako alitumia kadi ya simu iliyomilikiwa na Innocent Maiga bila kuripoti kwa mtoa leseni.
Shtaka la pili linamkabili Maiga ambaye anadaiwa kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya kadi ya simu.
Anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba mosi, 2019 na Mei 19, 2020 Mbezi Beach Kinondoni, kwamba kinyume na sheria alishindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya namba ya simu kama inatumiwa na Idris Sultan.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa walikana makosa yao na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Jamhuri hawakuwa na pingamizi kwa dhamana, hivyo washtakiwa waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili, waliosaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 15 kila mmoja.
Hata hivyo, Wakili wa Idris Sultan, Benedict Ishabakaki ameondolewa kumuwakilisha mshtakiwa huyo kwa sababu atatumika kama sehemu ya ushahidi wa Jamhuri kutokana na kushuhudia mteja wake akichukuliwa maelezo Polisi, hivyo anabakia Wakiki Jebrah Kambole.
Kesi imeahirishwa hadi Juni 9, kwa kutajwa.