30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

IBRAHIM RAMATU SIFIKIRII KUIKACHA KUNG FU KWA TAMAA YA FEDHA

Na SHARIFA MMASI-DAR ES SALAAM


KATIKA ulimwengu wa sasa wa michezo, wapo baadhi ya wachezaji wenye mapenzi na maamuzi magumu kama haya.

Unataka kujua ni maamuzi gani? Ni haya ya nyota wa timu ya taifa ya mchezo wa Kung Fu ‘Wushu’, Ibrahim Ramatu, aliyedai hajawahi kufikiria kuacha kuucheza mchezo huo kwa tamaa ya fedha.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 21, anakipiga katika klabu ya Shailin yenye makazi yake Tabata Relini, jijini Dar es Salaam, inayonolewa na kocha mchezaji, Ramadhan Mshana.

Ibra anayetokea katika kabila la Wapare huko mkoani Kilimanjaro na ni kijana pekee kwenye ukoo wao anayecheza mchezo huo.

SPOTIKIKI lenye desturi ya kupiga stori na mastaa wa michezo mbalimbali, leo limemnasa Ibrahim aliyefunguka mambo mbalimbali ndani na nje ya mchezo huo.

Spotikiki: Mwaka gani ulijikita rasmi kwenye mchezo huo na kwanini?

Ramatu: Mwaka 2010 ndio nilianza rasmi kucheza Kung Fu baada ya kuufuatilia kwa muda mrefu.

Spotikiki: Umesema kuufuatilia! Kivipi?

Ramatu: Moja ya njia kuu nilizokuwa natumia kuufuatilia huu mchezo ni kutizama video za mastaa mbalimbali waliowahi kutamba akiwemo marehemu Bruce Lee (Master of Kung Fu).

Spotikiki: Ilikuchukuwa muda gani kuifahamu Kung Fu kwa kina?

Ramatu: Mhhhh! Kwakuwa nilikuwa mfuatiliaji mzuri kupitia mitandao ya kijamii, haikunichukuwa muda mrefu, niliufahamu vema mchezo na kuanza kushiriki michuano mbalimbali ya ndani.

Spotikiki: Ulijisikiaje baada ya kuchaguliwa kuitumikia klabu yako kwa mara ya kwanza kupitia michuano ya taifa miaka iliyopita?

Ramatu: Nilijisikia faraja sana, nilijiona ni mwenye thamani kwenye familia nzima ya Kung Fu.

Spotikiki: Kipi kikubwa ulichojifunza kutoka kwa mkali huyo kinachokusaidia kukabiliana na mpinzani wako katika michuano mbalimbali unayoshiriki?

Ramatu: Nimejifunza mambo mengi sana, staili zote alizokuwa akizitumia huyu jamaa ndio ninazo mimi, najua kucheza na fimbo, mapanga na dhana mbalimbali.

Spotikiki: Ulishawahi kushiriki michuano nje ya nchi? Kama ni ndio, lini na wapi?

Ramatu: Naam nilishapata bahati hiyo, mwaka jana nilishiriki tamasha la kimataifa lililofanyika nchini China, nilifurahi na kuiwakilisha vema nchi yangu.

Spotikiki: Changamoto gani umewahi kukumbana nazo tangu uwe mwanafamilia wa Kung Fu?

Ramatu: Changamoto ni nyingi, kwanza kabisa kwa hapa nyumbani bado mchezo huu hauna mashabiki kama ilivyo soka, nafikiri kuna kila sababu ya viongozi wetu kuutangaza ili upate wadau wengi watakaokaribisha upinzani mkubwa.

Spotikiki: Manufaa uliyoyapata kupitia Kung Fu?

Ramatu: Nimenufaika na mambo mengi sana, kwanza uimara wa afya yangu kupitia mazoezi ninayofanya, pili nimeweza kusafiri nchi za nje, kujulikana na watu wengi na kuheshimika na jamii iliyonizunguka.

Spotikiki: Unajutia nini kwenye maisha yako?

Ramatu: Mhhh! Hakuna ninachojutia mpaka sasa, namshukuu Mungu kwa kila hali.

Spotikiki: Ukibahatika kupata watoto utakuwa tayari wajifunze mchezo gani?

Ramatu: Naam, hilo lipo katika kichwa changu muda wote, namwomba Mungu anijaliye na anipe mke mwema nitakayekuja kuzaa naye watoto ambao wote nitawaelekeza katika mchezo wa Kung Fu, kwani naamini watanufaika upande wa afya zao kupitia mazoezi mbalimbali watakayofanya.   

Spotikiki: Ushauri wako kwa vijana kuhusiana na mchezo huu.
Ramatu: Nawashauri vijana mbalimbali nchini wajitokeze kwa wingi kujifunza mchezo wa Wushu kwa manufaa ya maisha yao na taifa kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles