26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Huzuni Pluijm akiaga wachezaji

yanga*Yanga yamwajiri mtendaji Mfaransa kwa miaka mitatu

JENIFA ULEMBO na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA kocha mkuu wa Yanga, Hans Van der Pluijm, jana alitokea katika mazoezi ya timu hiyo kuwaaga wachezaji wake baada ya kujiuzulu, huku akiacha ujumbe mzito kwa mashabiki wa Yanga pamoja na wachezaji wa timu hiyo.

Pluijm aliwaachia ujumbe wachezaji akiwasihi kupendana, kujituma, kuwa na nidhamu, kuhakikisha wanapambana kutetea ubingwa wao pamoja na kuweka mbele masilahi ya timu.

Kocha huyo pia amewataka mashabiki washikamane pamoja na wasimame na timu yao ili iendelee kuwa imara.

 

Pluijm juzi jioni aliandika barua ya kujiuzulu kuitumikia timu ya Yanga, huku akisema hana wasiwasi wowote na maamuzi aliyoyafanya, kwani mlango mmoja ukifungwa mwingine hufunguliwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Pluijm aliwashukuru mashabiki wa Yanga kwa kuipa sapoti kubwa timu yao, huku akiwasisitiza kuendeleza mshikamano.

“Niwashukuru mashabiki wa Yanga kwa

ushirikiano mkubwa, niwaombe waendelee

kusimama na timu yao na si kusimama na

kocha, kwa kuwa kocha ni mtu  wa kuondoka

muda wowote,” alisisitiza Pluijm.

Akizungumzia kuondoka kwa kocha huyo, kocha wa makipa wa klabu hiyo, Juma Pondamali, alisema kuondoka kwa Pluijm ni pengo kubwa, kwani alikuwa ni miongoni mwa walimu bora hapa nchini.

 

Pondamali alisema daima mchango wa Pluijm utakumbukwa na kila mtu, kwani alikuwa na timu hiyo kwa kipindi kirefu na kufanikiwa kufanya vyema katika michuano ya kimataifa.

“Pluijm alikuwa ni mzuri sana, ameweza kuisaidia timu kufika mbali na kuonekana ni bora kimataifa, ambapo kwa kipindi cha miaka tisa haikuwahi kufanya vizuri.

Mshambuliaji Saimon Msuva, alisema kwa ujumla wachezaji wote wamesikitishwa na kitendo kilichotokea kwani walitamani kuendelea kuwa na kocha huyo.

“Siwezi kuzungumza mengi ila kwa ufupi nimeumia sana, kila mchezaji ameumia hakuna aliyefurahia hili lililotokea, ukiangalia mimi tangu nisajiliwe Yanga nimeweza kunolewa na makocha watatu tofauti, sitaki kuzungumzia waliopita ila Pluijm alikuwa tofauti, nilikuwa napata nafasi ya kuzungumza naye kumweleza yanayonisumbua na ananipa ushauri mzuri,” alisema.

Kwa upande wake, Amissi Tambwe alisema Pluijm ameondoka wakati bado anahitaji mchango wake.

“Nimeguswa sana na nina masikitiko makubwa kwa sababu nilimzoea na bado nilikuwa nahitaji msaada wake, lakini ndio maisha ya soka yalivyo, tunapaswa kukubaliana nayo,” alisema Tambwe.

Pluijm ameipa Yanga ubingwa wa ligi kuu mara mbili mfululizo katika msimu wa 2014/2015  na 2015/2016, aliipa Yanga ubingwa wa Ngao ya Jamii msimu wa  2015/2016 na Ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA).

Pia ameiwezesha timu hiyo kuingia hatua ya makundi (robo fainali) ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kumaliza hatua hiyo, ikiwa nafasi ya nne kwenye kundi lililokuwa na timu ya Mo Bejaia ya Algeria, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Madeama ya Ghana.

Wakati huo huo, Mfaransa Jerome Dufourg, ametangazwa kuwa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles