23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

HUYU NDIYE ‘MHALIFU’ ALIYEMPA USHINDI TRUMP?

alisa-shevchenko-russia-hacking-751388

NEW YOKR, MAREKANI

JINA la mlimbwende Alisa Shevchenko, limechukua sura mpya katika sakata la udukuzi uliosababisha kupanga matokeo ya uchaguzi nchini Marekani na kukinufaisha Chama cha upinzani cha Republican.

Uchaguzi huo ulifanyika Novemba 8 mwaka jana, ambapo wagombea wawili kutoka vyama mashuhuri walichuana vikali.

Hillary Clinton wa Chama cha Democrat ambaye amewahi pia kuwa waziri wa mambo ya nje katika awamu ya kwanza ya Rais Obama, alichuana na bilionea na mfanyabiashara mkubwa, Donald Trump wa Chama cha Republican.

Uchaguzi wa mwaka jana umesababisha doa kubwa kwa Serikali ya Barrack Obama pamoja na idara za ulinzi, usalama na ujasusi nchini humo, baada ya kuibuka madai kuwa Serikali ya Urusi ilifanya udukuzi na kuharibu mfumo wa matokeo ya uchaguzi huo kwa lengo la kumpa ushindi mgombea wa Republican.

Madai hayo yanaongozwa na Rais Obama, makamu wake Joe Biden na Chama cha Democrat ambao wameshirikiana na wakuu wa idara za usalama kukusanya ripoti zinazoonyesha namna Serikali ya Rais Vladimir Putin wa Urusi ilivyofanya uhalifu wa kimtandao na kuhujumu uchaguzi wa Marekani ili kumpa ushindi Trump.

Udukuzi ni uhalifu kwa njia ya mtandao ambao unalenga kupeleleza, kuiba taarifa, kubadili takwimu au rekodi na wakati mwingine kutumika kufanyia utapeli. Aidha, hutumika kuwafuatilia watu fulani wanaolengwa kwa nia nzuri au mbaya.

Katika muktadha huo, Alisa Shevchenko anatajwa kuwa mdukuzi aliyefanikisha kubadili matokeo ya urais wa Marekani na kumpa ushindi Donald Trump.

Alisa ameibuka kufuatia taarifa za kijasusi zilizotolewa na Ikulu ya Marekani, baada ya kampuni yake kuwekwa kwenye orodha zinazotakiwa kufutwa na kutofanya shughuli zozote nchini humo.

Aidha, Alisa anatajwa kuwa ndiye kinara aliyemsaidia Rais Vladimir Putin kuingilia mfumo wa mawasiliano wa Tume ya Uchaguzi ya Marekani

Alisa Shevchenko, anatajwa kuwa hodari katika matukio ya uhalifu wa kimtandao na mdukuzi mwenye ujuzi wa hali ya juu.

Kwamba amekuwa akitumika kubaini udhaifu wa utunzaji wa siri za kampuni kubwa za kibiashara, Serikali na taasisi mbalimbali nchini Marekani kupitia mtandao.

Mshangao mkubwa umetokea baada ya kampuni yake kutajwa kwenye orodha ya zinazotakiwa kufutwa mara moja kufanya shughuli nchini Marekani, ambapo serikali ya nchi hiyo imazitaja kampuni nyingine zisizotakiwa kuendelea kufanya kazi ndani ya mipaka yake.

Orodha ya kampuni zilizowekewa vikwazo kufanya kazi nchini Marekani ilitolewa wiki iliyopita kwa madai zilihusika kuvuruga uchaguzi kwa maslahi ya Urusi na kumpa ushindi Trump kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa mwaka jana.

Kampuni ya Alisa Shevchenko imetajwa kwa jina la ZOR, inadaiwa kutumika kama kitengo cha ujasusi cha Serikali ya Urusi. Aidha, inadaiwa kutumika kutoa ushauri wa kiufundi, utafiti na maendeleo kwa Serikali ya Shirikisho la Urusi.

Hatua hiyo ilimlazimu Alisa Shevchenko kupinga kitendo cha kampuni yake kuwekwa kwenye orodha hiyo, amedai kuwa hafahamu lolote na hajawahi kufanya kazi yoyote kwa niaba ya Serikali ya Urusi.

Alisa aliandika baruapepe kwenda kwa gazeti la The Guardian la England na kudai Ikulu ya Marekani imepotosha umma na huenda imefanya hivyo kama hila ili kushusha hadhi ya kampuni yake au namna nyingine yoyote mbaya dhidi yake.

Shevchenko alisema: “Mwanamke kijana na mdukuzi asiye na msaada wowote katika kampuni yake, anaonekana kama ndiyo mtu anayetumika na viongozi kuwadanganya wananchi ili wakamilishe nia yao. Siwezi kujificha, ninasafiri sehemu mbalimbali duniani na nimekuwa rafiki mzuri kimawasiliano na watu wangu.

“La muhimu, sina kiasi kikubwa cha fedha wala mamlaka au watu wanaofanya kazi nami nyuma ya pazia hadi nilaumiwe kiasi hicho. Kwa kweli mimi naweza kuwa mtu yeyote yule wa kawaida.”

Aidha, ameshutumu kiwango kikubwa alichokiita cha kijinga cha habari za udukuzi wa Urusi.

Hata hivyo, Donald Trump amepuuza ripoti za kiintelijensia zinazodai kuwa Vladimir Putin amemsaidia na kufanikisha ushindi wake kwenye uchaguzi uliopita.

Rais huyo mteule amesisitiza kuwa udukuzi wa Urusi hauna madhara yoyote wala haukuwa chanzo cha ushindi wake wa urais. Pia amepuuza madai ya kuwa mashine za uchaguzi hazikudukuliwa kama inavyoelezwa na Serikali ya Obama.

Trump ametoa msimamo huo ikiwa ni dakika 10 mara baada ya kukutana na Maofisa wa Usalama kuzungumzia kadhia hiyo ya Serikali ya Kremlin.

Rais huyo ameonyeshwa ripoti inayoelezea ‘agizo’ la Rais Putin kuingilia kampeni za uchaguzi mwaka jana kwa lengo la kuamua mshindi anayemtaka.

Uchunguzi wa sakata hilo umefanywa na Idara ya Usalama ya Marekani (NSA), Shirika la Upelelezi wa ndani (FBI) na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), ambayo kwa pamoja yalitakiwa kuthibitisha taarifa iwapo Putin aliingilia uchaguzi wa Marekani au la.

“Malengo ya Urusi yalikuwa kushusha imani ya wananchi kwa Chama cha Democrat, kumwangusha Hillary Clinton na kuvuruga mpango wake wa kuchaguliwa kuwa Rais,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti inabainisha kuwa Urusi iliingilia na kuwa na amslahi makubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana ikiwa na lengo la muda mrefu kuiporomosha serikali ya Chama cha Democrat nchini Marekani. Aidha, inasema malengo mengine yalikuwa kukabiliana na hatari zozote zilizoelekezwa kwa Urusi kama taifa na uongozi wa Putin.

Baada ya kupewa muhtasari huo, Trump alikataa madai kuwa ushindi wake ulipatikana baada ya kuingiliwa kwa mfumo wa Tume ya Uchaguzi.

Tathmini ya wana usalama hao haikutaja udukuzi uliofanywa kwenye baruapepe ya mwenyekiti wa kampeni ya Hilary Clinton, John Podesta.

Clinton alilalamika baada ya uchaguzi kuwa Putin ana ugomvi binafsi dhidi yake. Hata hivyo, hakueleza zaidi nini chanzo cha ugomvi huo.

Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin amepuuza tuhuma hizo na kudai Serikali ya Chama cha Demoicrat inatakiwa kuangalia matatizo yake badala ya kutafuta mchawi.

Akizungumza katika mkutano wa kufunga mwaka 2016, Putin alieleza: “Suala hili linatumika kuwahadaa wapiga kura, badala ya kuwaambia ukweli. Chama cha Democrat hakijashindwa kwenye nafasi ya urais pekee, wameshindwa kwenye Bunge la Kongresi na Seneti, je, huko nako ni kazi yangu kuwaangusha?

Putin aliongeza akisema: “Kuendelea kuwahadaa watu ni jambo baya. Kwa mfano, mmoja wa wagombea na Kiongozi wa Kamati Kuu ya Taifa ya Chama cha Democrat aliachia ngazi, wanatakiwa kuomba radhi kwa makosa yao si kusingizia wengine.”

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles