23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Huyu ndiye Glory Mziray aliyezimika

John Nchimbi

ILIKUWA ni siku ya kawaida kabisa ambapo hakuna tegemeo la kupata taarifa yoyote mbaya, nilipoona ujumbe mfupi kutoka kwa Julie Mziray, mdogo wa mwisho wa Meneja wa Habari wa Taasisi ya Misitu Tanzania ukisomeka kwa maneno mawili tu “Da Koku amefariki”.

Sina hakika kama akili yangu imekubali mpaka sasa kupokea taarifa hii hasa unapotambua Koku kama ambavyo familia yake imekuwa ikimwita alikuwa ni mzima wa afya, kama binadamu kuna wakati unapitia mambo magumu na ya kutisha lakini ni wazi aliyapita lakini kafikia tamati akiwa mwenye furaha na bila hata dalili ya kuumwa.

Kwa wale waliopata kuishi maisha ya Glory Walter Mziray, hasa maisha ya utotoni mkoani Morogoro, watabakia na kumbukumbu moja kubwa kuwa Glory alikuwa na kipaji kikubwa cha kuwa na marafiki, sina hakika aliwezaje kuwa na marafiki zaidi ya elfu moja na kila mmoja akiamini Glory ni rafiki yake wa karibu, akimpa kila mmoja tabasamu na nafasi ya kuweza kueleza masaibu yake, Glory alisimama kwa ajili ya watu na kwa ajili ya familia yake.

Sikumbuki kama amewahi kuhitilafiana na mtu kuanzia akisoma Shule ya Msingi Bungo na kumaliza elimu ya msingi mwaka 1989, baada ya hapo alifaulu kuingia Morogoro Sekondari mwaka 1990 ambapo alisoma mpaka kidato cha nne na kupangiwa kwenda kusoma kidato cha sita mchepuo wa HGL, Dakawa Sekondari. Safari yake ya elimu haikuishia hapo, alienda Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine na kusoma shahada ya kwanza ya uandishi wa habari.

Glory alikuwa ni mtu mwenye bidii na malengo, hivyo alirudi mjini Morogoro na kufanya kazi mwa takribani mwaka mmoja kama mwandishi wa habari na kuamua kujiunga na elimu ya Uzamili kwenye utawala wa Biashara (MBA).

Mara baada ya kuhitimu MBA yake mnamo mwaka 2004 ambapo thesis yake aliangazia zaidi mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali, alielekea mjini Arusha na kufanya kazi na Kampuni ya Farm Africa.

Glory alikuwa ni mtu mwenye kiu ya elimu na kujielimisha, kwa mara nyingine tena alijiunga kusoma shahada ya uzamili kwa mara ya pili, safari hii ilikuwa ni Chuo cha Mtakatifu Augustine akisomea mawasiliano ya umma.

Kwangu kuondoka kwake ni jambo lenye huzuni kubwa, nimekuwa naye shule ya msingi pamoja, tukawa tena Morogoro Sekondari pamoja, baada ya hapo nikamshawishi tukaenda Mzumbe kufanya shahada ya uzamili pamoja na alipohamia Arusha alinikuta mimi nikiwa nimetangulia kama miezi sita na baadaye akanishawishi na mimi nikasoma shahada ya uzamili tena ya mawasiliano ya umma.

Kwa waliobahatika kufanya naye kazi watakumbuka kuwa ni mtu anayeamini sana kuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi wenzake, lakini pia alipenda kutosema mawazo yake hasa inapokuwa mawazo yake hayawezi kubadili kitu tena kwa wakati huo.

Sifa yake kubwa ni kusimamia kile anachokiamini kwa nguvu zote na hata kwa miaka mingi. Glory akiamua kwenda mbele alikuwa hageuki kirahisi. Anamaanisha anachokifanya na akikata shauri basi hiyo ndiyo njia atakayopita.

Marafiki na tasnia ya waandishi wa habari hasa wa Morogoro siku zote watamkumbuka Glory kama rafiki wa wote, hajui kumdharau mtu kwa uwezo au cheo chake, kwake watu wote walistahili kuheshimiwa.

Glory Mziray, mama wa Dishon na Hellen, dada wa Alex na Jullie, uzao wa kwanza wa Walter Mziray na Mama Angel. Hakuna jambo jepesi wala faraja kuu kwa familia na hasa watoto kumpoteza mama yao.

Lakini kwa imani yetu na kuzingatia kuwa ni Mkristo, basi tunaamini Mungu hajawaacha peke yao. Basi kupitia kwetu na tumkimbilie yeye kwenye nyakati hizi ngumu kwa maana Biblia inatuhusia; “Mtegemeeni nyakati zote. Mimineni moyo wenu mbele zake. Mungu ni kimbilio letu.” (Zaburi 62:8).

 Wakati huu ambao ni mgumu kabisa na hakuna matumaini, wakati ambao mioyo imepondeka kwa maumivu basi tunakumbushwa kuwa kipindi ambacho kila mmoja wetu anatamani walau angepata nafasi ya kusema neno moja kwa familia, kwa watoto wake aliokuwa akiwapenda sana ni wazi tumekwishachelewa lakini kimbilio letu ni kwenye Neno la Zaburi 147:3  “Anawaponya wenye mioyo iliyovunjika, naye anafunga sehemu zao zenye maumivu.”

Hakuna aliyejiandaa leo kuwa bila Glory, si watoto wala wafanyakazi wenzake, kwa sasa maisha ni kama giza kwa mbele na hakuna nuru ya mwanga, Dishon na Hellen, wana hofu kwa kuwa wanaanza maisha mapya bila mama.

Mwenyezi Mungu anajua kila mtu ana hofu, hofu ya kuanza maisha mapya bila dada, binti au rafiki, bila mama wa kusema nishauriane naye kama mama wa watoto lakini tushike moyo na kumbuka kuwa Mungu anasema kwenye Isaya 41:13. “Usiogope. Mimi mwenyewe nitakusaidia.”

Tupeane faraja kwa neno la kweli na uzima linalotuhusia kuwa walioaga dunia wakiwa na amani hawajafa bali wamelala wakisubiri siku ya mwisho. Nao wataanza kwanza kuamka na kulaki ufalme wa Mungu kabla ya watakaokutwa hai 1 Wathelasonike 4:15; “Kama alivyosema Bwana mwenyewe, tunawaambieni kuwa sisi ambao tuko hai bado, tutakaokuwa hai mpaka Bwana arudi, kwa hakika hatutawatangulia wale waliokwisha kufa.

Waliokufa wakiwa na imani basi nao wataona mikono ya Mungu kupitia kusulubiwa msalabani kwa Yesu Kristo kulikoleta ukombozi, kwa maana kwa  sheria (torati), wote tu wadhambi  hivyo hatutahesabiwa haki kwa sheria bali tutahesabiwa haki kwa neema ya Mungu.

Kwa manaa kama ni kwa sheria hakuna mmoja wetu atakayeona mbingu ila kwa neema ya Mungu Warumi 3:21-26: “Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii na haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio.

Maana hakuna tofauti, kwa sababu wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa.

Binafsi nimekujua Glory kama mtu wa karibu kwangu miaka 30 iliyopita, yatosha kusema ulikuwa mtu mwema sana na pale unapopata ushauri sahihi hujawahi kufanya makosa.

Nilikuwa najua kuna muda bado wa kuwepo duniani, kumbe sikuwa sahihi kwa maana kifo ni fumbo la ajabu sana. Kuna mambo mapya bado nilikuwa sijakushirikisha na kuyazungumza kwa mapenzi ya Mungu umeniweza, nakuondoka bila ya kwaheri, lakini kwa uhakika hapo ulipo sasa unaona kila jambo na kujua kila kitu cha hapa duniani, sina shaka una furaha kuona kuwa sisi tuliobakia ni marafiki wema na wa kweli toka zamani mpaka sasa.

Glory amepigana vita vilivyo vizuri, mwendo ameumaliza na imani umeilinda kwani kufa ni faida na kuishi ni Kristo. Upumzike kwa amani mpaka tutakapoonana tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles